29 October 2010

Mtandao wa makanisa wachakachuliwa.

*Ujumbe wa kueneza udini wasambazwa.

Na John Daniel
JUKWAA la Kikristo Tanzania limelaani vikali kitendo cha watu wasiojulikana kuhujumu mtandao wao wa mawasiliano ya barua pepe unaotumiwa na Jumuiya ya Makanisa ya
Kipentekoste Tanzania (PCT), na kusambaza ujumbe wa uwongo unaolenga kuwagawa Watanzania kidini.

Pia Jumuiya hiyo imewaomba Watanzania kupuuza taarifa zilizochapishwa na magazeti mawili jana (si Majira) zikidai kuwa wakristo wanamtaka rais wa dini hiyo, kwa kuwa ni za uongo na zinalenga kuvuruga Uchaguzi Mkuu ujao.

Wakisoma tamko la kulaani hujuma hizo Dar es salaam jana, Makatibu wakuu wa Jukwaa hilo walisema wamesikitishwa na taarifa hizo za uongo na kuomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa haraka juu ya hujuma hizo.

"Kufuatia habari katika magazeti...napenda kuweka bayana kuwa taarifa ya email iliyotumiwa kuandaa habari hiyo ni ya uongo na haikuandikwa na mimi Katibu Mkuu wa PCT na wala Jumuiya haihusiki.

Napenda kuweka wazi kuwa tumeingiliwa mawasiliano yetu ya email (barua pepe) ambapo email yetu imetumika kutuma ujumbe wenye uchochezi kwa umma wa Watanzania, hii ni hujuma kubwa kwa Jumuiya ya Kipentekoste na wakristo kwa ujumla," alisema Askofu David Mwasota, Katibu Mkuu PCT.

Aliongeza kuwa, "PCT inalaani kitendo hicho na tunaliomba Jeshi la Polisi kushughulikia mara moja ili kuepusha udini katika taifa letu, mpango huu umelenga kuwanufaisha wasiopenda amani kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuwagawa Watanzania," alisisistiza.

Alisema PCT inakanusha habari zilizoandikwa katika vyombo hivyo kwa kuwa ni za kupotosha umma na zinalenga kuvuruga Uchaguzi Mkuu kwa kuingiza suala la udini huku zikinufaisha upande mmoja.

"Tunapenda kuwaambia wakristo wote pamoja na jamii ya Watanzania kuwa taarifa hizi za upotoshaji si za kweli na haziwahusu wakristo kwa ujumla wake, wale wanaohusika kuziandika habari hizi wana nia mbaya ya kutugonganisha sisi wakristo kwa wakristo, wakristo na serikali yao, wakristo na vyama vya siasa na wakristo na watu wa dini nyingine.

Tunaomba wakristo na watanzania wote kwa ujumla wawaogope waaandishi wa habari za jinsi hii," alisema Askofu Mwasota.

Viongozi hao pia waliwaomba wakristo wote kuhudhuria ibada zao siku ya Oktoba 31 kama ilivyopangwa na viongozi wao katika makanisa husika na baadaye wahakikishe wanapiga kura baada ya ibada kwa kuwa ni haki yao kufanya hivyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Padri Anthony Makunde alisema baada ya kiongozi wa chombo kilichochapisha habari hizo za uongo yeye mwenyewe alifika ofisi zao lakini alikaa zaidi ya dakika 30 bila kupewa uthibitisho wa habari hizo kama walivyokuwa wamedai.

Alisema walisikitishwa na chombo hicho kuchapisha habari hizo bila hata kutafuta upande wa pili jambo linalowahakikishia kuwa hizo ni hujumu zinazolenga kuwavuruga Watanzania kwa kujenga dhana ya udini.

Naye Katibu Mkuu Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Dkt. Leonard Mtaita alisema wamesikitishwa na taarifa hizo na kuhoji uhalali wa baadhi ya watu kutumia vibaya jina la wakristo bila ushaidi.

1 comment:

  1. Kufuatia msimamo wa viongozi wa dini wa Kikristo kukanusha matumizi mabaya ya mtandao wao na chombo cha habari husika kujitwalia habari habari potofu ni dhahiri maadili ya uandishi yamekiukwa. Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Waandishi wanapaswa kufuatilia kwa karibu taarifa hiyo ili kuimarisha maadili ya kazi na kudumisha mustakabali wa amani ya nchi yetu. Chombo husika kinapaswa kuona kuwa Watanzania ni wa -moja bila kujali imani, rangi au wapi mtanzania anakotoka.

    ReplyDelete