28 October 2010

Mpango wa Maghembe wadaiwa ni kutapatapa

Tumaini Makene na Reuben Kagaruki

HATUA ya Waziri wa Elimu na Mafunzo Stadi, Profesa Jumanne Maghembe, kusema kuwa suala la elimu bure ni sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa iwapo chama
hicho kikichaguliwa kinapanga kubadili mfumo ili kuifanya elimu ya msingi iwe kuanzia awali mpaka kidato cha nne, imezua mjadala huku ikielezwa kuwa ni dalili za kutapatapa na kuelemewa kwa chama hicho na serikali yake iliyoko madarakani sasa.

Mmoja wa wanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kuwa maelezo ya Prof. Maghembe yanapaswa kutiliwa shaka kwani Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni mgombea urais wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ameshakataa katika mikutano yake ya hadhara kuwa serikali haiwezi kutoa elimu bure.

"Unajua hii ni dalili ya serikali na CCM kwa ujumla kutapata, hawa watu wanaonekana hawako coordinated (wameparaganyika), yaani huyu anasema hili leo, mwingine anasema hivi kesho na yule anasema vingine tena, wote wamekuwa wakikataa kuwa suala la elimu bure haliwezekani, Kikwete kasema hivyo akiwa Kigoma kwenye mkutano wa kampeni, Spika Sitta (Samuel) alikataa, CCM imeshasema mara kadhaa, sasa huyu vipi, ni dalili za kutaka kuiba sera za wenzao...sasa wameishiwa," alisema mwanzuoni huyo ambaye ni mhadhiri mwandamizi.

Aliongeza "ukiona serikali inazungumzia suala moja lakini ikatoa majibu au hoja tofauti tofauti hiyo ni dalili ya kutapata, wanapingana wao kwa wao sasa."

Mwanazuoni mwingine na mmoja wa wachambuzi mahiri nchini, Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, alisema kuwa tamko la Prof. Maghembe linadhihirisha jinsi ambavyo CCM imekuwa 'ikirukia' hoja za wapinzani na kutaka kuziteka, baada ya kushindwa kutetea hoja zake mbele za wananchi.

"Sasa huyu Profesa mbona anashangaza, wenzake wote akiwemo Kinana (Abdulrahman), nilikuwa naye kwenye mdahalo, alisema hili suala la kutoa elimu bure haliwezekani, sasa wameona wameshindwa kutetea hoja zao mbele ya wananchi, wameamua kutuunga mkono, wakijifanya ni ya kwao, ni mbinu ile ile, if you cant defeat them join them (kama huwezi kuwashinda bora uungane nao), hata wazo la kuifanya Dodoma kuwa kituo cha elimu na kujenga University of Dodoma, walichukua katika ilani yetu, lakini hawakuwa nayo.

"Hii inadhihirisha kuwa kumbe CHADEMA kinapaswa kuchaguliwa sasa na si wao wanaoiga...maana sasa wanaonekana kuelemewa kabisa, wameona hoja yetu ya elimu bure inawagusa Watanzania wote huku hoja za CCM kupinga zikipuuzwa na wananchi... inakuwaje Profesa anaamua kuzungumzia kitu ambacho hakipo katika ilani ya chama chake, wanarukia hoja...lakini it is too late (wamechelewa), wao wakubali tu waondoke...kwenye madini kazungumza Ngeleja, Afrika Mashariki kazungumza Kamala, Membe tayari, Wassira pia, watazungumza wangapi maana hoja zetu zimekubalika karibu kila sekta," alisema Prof. Baregu ambaye pia ni Meneja Kampeni wa CHADEMA.

Mbali na wanazuoni hao, wadau wengine wa elimu waliozungumza na Majira walisema kuwa duniani kote utaratibu anaopendekeza Profesa Maghembe haupo.

"Hakuna utaratibu wa aina hiyo duniani kote... haiwezekani watu kusukumwa kwenda mbele bila kuwafanyia tathmini," alisema mmoja wa wadau wa elimu, Bw. Nyanda Shuli akiitaka serikali kabla ya kutafakari kuanza utaratibu huo irejee madhara yaliyopatikana baada ya kuondoa mtihani wa darasa la nne.

"Wadau wengi wamefanya tafiti na kubaini wanaomaliza kidato cha nne bila kusoma na kuandika...mtihani huu ulisaidia kuhamasisha watoto wasome na haikuwa kwa lengo la kuwatisha... lakini leo hii tukisema asukumwe hadi kidato cha nne tutakuwa tunasaidia nini?" alihoji Bw. Shuli ambaye ni ofisa katika Shirika la HaliElimu, aliyekuwa anatoa mawazo binafsi.

"Nimeenda hadi vijijini kule Rorya kuna watoto wanahitimu kidato cha nne bila kujua kusoma, tatizo lipo watu wanajiuliza tatizo ni nini," aliongeza.

Mbali ya wanazuoni hao na wadau mbalimbali wa elimu kupingana na tamko hilo, uchunguzi wa Majira pia umeonesha kuwa suala la elimu kuwa ya bure na kuwa itafanyiwa upanuzi ikiwemo kufanya mabadiliko ya utaratibu wa elimu ya msingi kuanzia awali mpaka kidato cha nne, badala ya darasa la saba la sasa, halimo katika ilani ya uchaguzi ya CCM.

Prof. Maghembe alikaririwa jana akisema kuwa serikali inapanga kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu nchini, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba kuendelea na kidato cha nne bila kuchujwa, akimaanisha kuwa ukomo wa elimu msingi kwa Tanzania utakuwa kidato cha nne kuanzia mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment