Na Elizabeth Mayemba
MAKAMU Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Davis Mosha amewataka wanachama na mashabiki wake kuondoa hofu, kwa matokeo mabaya yaliyojitokeza katika mechi tatu mfululizo na
kuwataka kutulia katika kipindi hiki, kwani bado wananafasi.
Yanga katika mechi zake tatu mfululizo, imejikuta ikitoa sare hali iliyosababisha kupigwa kumbo kileleni na wapinzani wao wa jadi Simba ambao sasa wameshika usukani wa ligi hiyo, huku wao wakishuka nafasi ya pili.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mosha alisema hakuna aliyefurahishwa na sare hizo, kwani lengo lao lilikuwa ni kupata pointi tatu kila mechi, hivyo hivyo watajipanga upya na kuhakikisha hali hiyo haijitokezi tena.
"Pia nawasihi wachezaji wetu, wasibweteke na ule ushindi walioupata kwa Simba, badala yake kila mechi wanatakiwa kuipa umuhimu," alisema Mosha.
Alisema kwa kuwa mzunguko wa kwanza ndiyo umefikia ukingoni, watakaa na kuangalia nini tatizo katika kikosi chao na kukifanyia marekebisho haraka, kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili.
Mosha alisema katika kipindi hiki, mashabiki wanatakiwa wawe watulivu na kutoa ushirikiano kwa uongozi, ili kumnyima nafasi adui, ambaye atataka kuhatarisha amani ndani ya klabu hiyo.
Alisema maadui zao wataona hii ndiyo nafasi ya kupenyeza migogoro yao, ili timu yao iendelee kufanya vibaya na kuwaomba wana-Yanga, wasitoe nafasi kwa watu kama hao.
Yanga imebakiwa na mechi moja, dhidi ya Toto African ya Mwanza itakayopigwa Novemba 7, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment