29 October 2010

Five Stras kuzindua mbili kwa mpigo leo.

Na Mwandishi Wetu

KUNDI la muziki wa taarab la Five Stars Modern, leo litazindua albamu mbili mpya katika ukumbi wa New Msasani Club, jijini Dar es Salaam. Bendi hiyo iliyotamba na
albamu yake ya kwanza ya Riziki Mwanzo wa Chuki iliyozinduliwa mwaka jana, itazindua albamu za Shukrani kwa Mpenzi na Ndio Basi Tena.

Katika uzinduzi huo, msanii mkongwe wa kimataifa wa muziki huo,  Fatuma Baraka, Omary Tego na kundi la Offside Trick, watawasindikiza kwa kuimba nyimbo zao mpya na zile zilizotamba zamani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa bendi hiyo, Ally Juma 'Ally J', alisema wasanii hao wamepanga kufanya mambo makubwa, baada ya kujiandaa kwa muda mrefu.

"Hawa wameahidi kufanya mambo makubwa, na wamejiandaa vizuri sana kuhakikisha wanawakamata mashabiki wa muziki wa taarab," alisema.

Alizitaja nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Shukrani kwa mpenzi uliobeba jina albamu, Dunia, Bibi wizi mtupu na Hanishushi na albamu ya Ndiyo basi tena, ina nyimbo za Ndiyo basi, Ukisema cha nini, La uchungu na Paka mapepe.

"Tumejiandaa vizuri na tuna uhakika mashabiki wa taarab watafurahia nyimbo zetu kama ilivyokuwa katika uzinduzi wa albamu ya kwanza ya Riziki mwanzo wa chuki," alisema.

Alisema katika uzinduzi huo,  kiingilio kimepangwa kuwa sh. 7,000, ili mashabiki wa muziki wa taarab waweze kushuhudia kwa wingi na kila mmoja atapata kanda ya kaseti moja bure.

Uzinduzi huo umedhaminiwa na gazeti la Dar Leo na Majira yanayochapishwa na kampuni ya Business Times Limited (BTL).

Mageziti mengine yanayotolewa na kampuni hiyo ni Spoti Starehe na Business Times na kituo cha redio cha 100.5 Times FM.

No comments:

Post a Comment