Na Kulwa Mzee
AHADI ya mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa ya kupunguza gharama za saruji na mabati kwa ajili ya kurahisisha ujenzi imeibua hamasa kwa
wapiga kura katika maeneo ya Jimbo la Ukonga na kuamua kuweka wazi kwamba kura ni siri lakini wanampigia atakayewakomboa katika shida ya kupanga nyumba.
Hayo yalibainika jana mitaani maeneo mengi ya jimbo hilo wakati wananchi wakienda na kutoka kupiga kura.
Kauli hiyo walikuwa wakiitumia wakati walipokuwa wakiulizana na hata mwandishi alipohoji baadhi ya wapiga kura kupata maoni yao, baadhi walisema wangempigia Dkt. Slaa kwa sera yake ya makazi na wengine Rais Jakaya Kikwete kwa hofu kuwa rais akitoka upinzani hakutakuwa na amani.
"Tumechoka kupanga, lazima tumpe kura Slaa, watu wengi huku maeneo ya ubena Gongolaboto watampa Slaa, simenti (saruji) mfuko sh. 5,000 na bati 6,000 kwa nini tusimpe atukomboe?" alisema mwanamke mmoja aliyejitambulisha kama Mama Esther aliyekuwa akienda kupiga kura huku kabeba mtoto.
Hali ya vituo vya kupigia kura maeneo ya Kitunda, Kivule, Gongolamboto, Mombasa, Pugu, Chanika na Mvuti ni shwari hakuna matatizo makubwa yaliyojitokeza japo kuna baadhi ya vituo vichache walichelewa kuanza kupiga kura kwa sababu ya karatasi kuchelewa.
No comments:
Post a Comment