01 November 2010

Kasoro zatawala uchaguzi Mkuu.

*Majimbo saba yashindwa kupiga kura
*Polisi anaswa na shahada  mkobani
*Wachana shahada kwa kukosa majina
*Mabomu ya machozi yatumika M'nyamala  

Na Waandishi Wetu Dar na mikoani
UCHAGUZI Mkuu wa rais, wabunge, wawakilishi na madiwani
umefanyika jana kote nchini huku ukitawaliwa na kasoro mbalimbali zikiwemo ukosefu wa vifaa, kukosewa karatasi za kura, vitendo vya rushwa na malalamiko kadhaa kutoka vyama vya siasa hatua iliyosababisha majimbo saba kuahirisha shughuli hiyo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kuahirisha uchaguzi wa wabunge katika majimbo matatu ya Tanzania Bara na manne Zanzibar kutokana na tatizo la upungufu wa karatasi za kupigia kura mbali na hilo iliahirisha uchaguzi wa madiwani katika kata 23 kutoka Halmashauri 13 Tanzania Bara.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam juzi jioni na kusainiwa na Mkurugenzi wa NEC, Bw. Rajab Kiravu ilieleza kuwa uchaguzi wa wabunge katika majimbo ya Nkenge, Mpanda Mjini na Mpanda Vijijini umeahirishwa.

Majimbo mengine ambayo chaguzi zake zimeahirishwa ni pamoja na Mwanakwerekwe, Mtoni, Magogoni na Wete huko Zanzibar. Taarifa hiyo pia ilizitaja kata ambazo chaguzi zake zimeahirishwa kuwa ni pamoja na Mtonya (Newala), Endegikot (Mbulu), Kisiwani (Same), Mji Mwema (Njombe), Itaraka (Manyoni), Kigwa na Ibelamikundi (Uyui).

Nyingine ni Msongezi (Ulanga), Kimuli na Kamuli (Karagwe), Kisanga (Sikonge), Mkutuni na Mirongo (Mwanza Jiji) Kitagata (Kasulu), Buseresere (Chato), Janga (Kibaha), Kibiti, Chemchem, Ngorongo, Kipungira na Mjawa (Rufiji).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchaguzi wa rais na madiwani uliendelea kama kawaida katika majimbo ambayo uchaguzi wa wabunge umesitishwa. Vile vile katika Kata ambazo uchaguzi wa madiwani umeahirishwa, uchaguzi wa rais na wabunge pia uliendelea kufanyika kama ulivyopangwa.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, tarehe ya kufanyika chaguzi hizo itatangazwa  baadaye na NEC.

  Wenyeviti CCM wahojiwa TAKUKURU

Katika tukio lingine Mwenyekiti wa CCM Tawi la Gezaulole, Bw. Hashim Ali na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbwamaji, Kigamboni, Bw. Ali Kiwi jana walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kugawa rushwa kwa wapiga kura.

Maofisa wa TAKUKURU waliwaweka chini ya ulinzi viongozi hao, kuwahoji na kuchukuliwa maelezo na baadaye kuwaachia. Mbali na watu hao, askari polisi mwenye cheo cha sajini  Marystelle Soko mkazi wa Manispaa ya Moshi anashikiliwa na polisi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kukutwa na Shahada sita za wapiga kura kinyume cha sheria.

Akizungumza na Majira, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Bw. Lucas Ng’hoboko alisema askari huyo alikamatwa juzi saa 11 jioni eneo la Mlandege Kata ya Bomambuzi akiwa na shahada hizo ndani ya  mkoba wake.

Alisema askari huyo alikamatwa baada ya polisi kupata taarifa za siri za kuwepo shahada hizo zinazodhaniwa kuwa zimenunuliwa kutoka kwa wamiliki wake halali.

Bw. Ng’hoboko alisema askari huyo wa kitengo cha Upelelezi alikamtwa na kupekuliwa kutokana na taarifa za siri zilizomtaja kwamba ameshiriki shughuli haramu la kununua shahada hizo.

“Tunamshikilia Sajini Marystella na tunaendelea kumuhoji kwa muda ili kujiridhisha na baadaye tufuate taratibu za kumchukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

  CCM yaridhia mwenendo wa uchaguzi

Naye Mwandishi wetu kutoka Dar es Salaam anaripoti kuwa Meneja  Kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Abdulrahman Kinana amesema licha ya kuwepo dosari ndogo ndogo za hapa na pale kwenye uchaguzi ameridhika na mwenendo wa upigaji kura jana.

"Kwa ujumla nimeridhika na mwenendo mzima wa uchaguzi hadi sasa, mbali ya kuwepo taarifa za vurugu zilizoanzishwa na wapinzani.
Kasoro nyingine ndogo ndogo za baadhi ya watu kukosa majina yao zilifanyiwa kazi na wahusika, lakini pia tusisahau kuwa kazi hii inasimamiwa na watu inaweza kuwa na mapungufu madogo madogo," alisema Bw. Kinana na kuongeza, "Tutatoa taarifa kamili kadri siku zinavyokwenda kati ya kesho (leo) na kesho kutwa.

Wakati hali ikiwa hivyo Tanzania Bara, kwa upande wa Zanzibar, hasa Unguja, upigaji kura ulifanyika kwa amani, licha ya kujitokeza kasoro ndogo kwa baadhi ya majimbo.

Majimbo yaliyokumbwa na kasoro hizo ni pamoja na Mtoni, Kwamtipura na Amani ambapo inadaiwa kujitokeza watu kupiga kura kwenye maeneo yasiyo yao,  wengine kupiga kura mara mbili na wengine kushindwa kuona majina yao.

   Wawili wachana shahada

Wilayani Kinondoni, wanawake wawili wakazi wa Manispaa ya Kinondoni, walichana shahada zao za kupigia kura baada ya kukosa majina yao katika vituo vya kupigia kura. Wanawake hao waliofahamika kwa jina moja moja la Bi. Halima na Mama Baraka walifikia uamuzi huo katika vituo vya Kambangwa na Msisiri

Kwa mujibu wa Bi. Halima, walifikia uamuzi huo baada ya kusumbuka kwa muda mrefu kutafuata majina yao bila mafanikio huku wakikosa  ushirikiano kutoka kwa mamlaka husika.

Alisema amekuwa akifuatilia jina lake katika kituo  hicho kwa siku nne mfululizo bila mafanikio ndipo aliamua kuchana shahada hiyo kwa madai kuwa  haina umuhimu tena kwake.

  Polisi warusha mabomu

Watu wawili wamejeruhiwa baada ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kurusha  mabomu matatu katika harakati za kutuliza ghasia katika kituo cha kura cha Mwananyamala Mchangani.

Sakata hilo liliibuka baada ya wakazi wa eneo hilo kugoma kusogea mbali na kituo hicho kwa madai ya kulinda kura na kuzuia mamluki.

Majira lilishuhudia wananchi hao wakigoma kuondoka katika kituo cha kupigia kura baada ya magari mawili yenye vioo vya giza kuingia kituoni hapo na kuibua hisia za kuwepo hujuma.Kutokana na hali hiyo polisi waliokuwa kwenye gari lenye namba PT 0987 walirusha mabomu matatu ya machozi yalimjeruhi Bi. Fatma Twaha mgongoni.

Ilidaiwa kuwa awali magari yalizuiliwa kuingia ndani ya kituo lakini walishangaa kuona gari hiyo Toyota Coster yenye vioo vyeusi, ikiruhusiwa kuingia hivyo kuibua hisia za hujuma kwa wananchi hao.

Polisi waliwatangazia wananchi kusogea umbali wa mita 200 kutoka kituoni jambo walilopinga. Hali ya wasiwasi iliendelea kutawala eneo hilo ambapo saa 9:35 alasiri polisi waliongeza magari likiwemo la upupu na kufanya jumla ya magari nane kila gari likiwa na zaidi ya askari nane.

Kutokana na hali hiyo, wananchi waliamua kutii amri na kusogea  hata hivyo vijana hao walirudi tena jirani na kituo hicho baada ya magari hayo kuondoka.


  Abambwa na furushi la kura

Mwanamke ambaye hakufahamika jina lake alinusurika kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira, baada ya kutuhumiwa kubeba furushi la kura zilizopigwa pamoja na pesa taslimu.

Chanzo cha habari kililiambia Majira kuwa baada ya wakazi wa eneo hilo kumshtukia, mama huyo aliamua kuingia katika msikiti wa Mwananyamala 'B' Kinondoni jijini Dar es salaam  lakini wakazi hao walimsubiri hadi alipotoka.

Baada ya kutoka msikitini, wakazi hao walimkamata na kumpekua ambapo walimkumkuta na furushi la kura zilizopigwa ambapo ilidaiwa alikuwa akizipeleka katika kituo cha kura cha Makumbusho.

Wakazi hao waliamua kumpeleka kituo cha Polisi Minazini na baadaye kuhamishiwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw. Elias Kalinga alikiri kupokea taarifa hizo na kuongeza kuwa kwa wakati huo hakuwepo ofisini.

Katika tukio lingine mgombea udiwani kata ya Kinondoni kupitia CHADEMA Bw. Deo Mushi jana alishikiliwa na polisi baada ya kuvamia kituo cha kupigia kura cha Kumbukumbu akiwa na sare za chama hicho na kudaiwa kuzua tafrani.

Bw. Mushi ambaye alifikia kituoni hapo kwa madai ya kumfuatilia kijana aliyedaiwa kugawa pesa kituoni hapo alikamatwa na pamoja na kijana huyo na kupelekwa kituo cha Oysterbay kuhojiwa na baadaye kuachiwa. 

Habari hii imeandaliwa na  Elisante Kitulo, Mwajuma Juma, Martha Fataely, Heckton Chuwa, Theonestina Juma, John Daniel na Yusuf Katimba.

No comments:

Post a Comment