01 November 2010

CHADEMA yalalamikia polisi Bukoba.

Na Tumaini Makene

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelaani Jeshi la Polisi mkoani Kagera kumshikilia mgombea ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Bw. Wilfred Lwakatare
, usiku wa kuamkia siku ya kupiga kura.

Pia chama hicho kimeendelea kulia na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutokana na kasoro zilizojitokeza katika mchakato wa uchaguzi jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja wa Kampeni wa CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu alidai kuwa Bw. Lwakatare, alikamatwa pamoja na wanachama wenzake baada ya kuvamiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Lwakatare amelala ndani usiku wa kuamkia leo (jana), amekamatwa na polisi jana usiku, ilikuwa baada ya kukutana na mawakala wake wakati wanaondoka njiani wakakutana na vijana wa CCM, green guards, wakawapiga, lakini cha kushangaza vijana hao hawakukamatwa badala yake wakakamtwa waliopigwa.

"Tunalaani kitendo hicho. lakini pia tunasikitishwa na taarifa zinazozidi kutufikia kutoka kwa wananchi juu ya kasoro mbalimbali kama vile watu kutokuona majina yao vituoni, pia ile namba ya simu ya NEC inayotumika kuuliza taarifa za wapiga kura haifanyi kazi, imelala," alidai Prof. Baregu.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Henry Salewi alisema hana taarifa za Bw. Lwakatare kulala ndani na akamtaka mwandishi kumuuliza mgombea huyo.

Alisema chama hicho kinasikitishwa na tukio la wananchi wa Mbeya mjini wakiwemo watoto wadogo kupigwa mabomu ya  machozi na polisi mkoani humo.

Alimwomba Mkuu wa Jeshi hilo (IGP) Said Mwema, kutoa maagizo juu ya kupunguza matumizi ya nguvu bila sababu za msingi katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

"Kwa sababu mpaka sasa tunazo taarifa kuwa kuna maeneo ambayo sisi tunaonekana kuwa na ushawishi, nguvu za ziada za vyombo vya dola zitatumika, tukio la Mbeya mjini likiwa ni mojawapo na maeneo mengine kama vile Sumbawanga, Arusha, Nyamagana, Iringa mjini," alisema Prof. Baregu

Aliomba NEC na polisi kuhakikisha kuwa kasoro zinazojitokeza zinatolewa ufafanuzi ili kuondoa dhana kuwa kuna hila zinafanyika katika kuvuruga mchakato wa uchaguzi kwa maslahi yasiyojulikana.

Pia alilalamikia baadhi ya vyombo vya habari kurusha vipindi vyenye kuashiria mwendelezo wa kampeni licha ya mchakato huo kumalizika na kuitaka NEC kuingilia kati suala hilo.

"Tunaisaidia NEC ili ionekane imesimamia uchaguzi halali," alisema.

Aliitaka Tume hiyo kuwa makini na karatasi za kura zilizoongezwa ili zisitumike isivyo wakati wa majumuisho, kutofautisha na kura halali zitakazopigwa vituoni.

No comments:

Post a Comment