28 October 2010

Amani Karume apewa ngao ya amani.

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume jana aliagwa na wananchi wa Zanzibar na kukabidhiwa Agao ya Amani ya Uongozi uliotukuka yeye na
mkewe, zenye thamani ya sh. milioni 45.

Hafla hiyo ya kuagana iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar, iliandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na mabalozi waliopo nchini.

Akitoa shukrani zake kwa wananchi, Rais Karume alisema kuwa  Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoundwa mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, inahitaji kufuata misingi ya amani na utulivu.

Alisema kwamba serikali hiyo ni muhimu sana katika kuendeleza umoja wa Wazanzibari nchini.

Hata hivyo, Rais Karume alisema kuwa kazi yote aliyoifanya katika kipindi cha miaka kumi hakuifanya peke yake, bali kwa kushirikiana na viongozi wenzake pamoja na wananchi wa Zanzibar.

“Nashukuru sana kupata zawadi hii, lakini kama ningaliulizwa kuhusu matumizi ya pesa hizi ningalishauri isomwe dua, yatungwe na mashairi na pesa zitakazobakia wapewe watoto yatima, lakini kwa kuwa nimepewa nashukuru sana,” alisema Rais Karume.

Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bw. Abdallah Mwinyi Khamis alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wameamua kutoa zawadi hiyo kwa rais kutokana na kuthamini mchango wake katika kuiletea maendeleo nchi.

Jumla ya sh. milioni 65.2 zilikusanywa kutoka kwa taasisi binafsi, serikali pamoja na vyama vya siasa na watu binafsi ili kufanikisha tuzo hiyo.

Waliochangia fedha hizo ni CCM, CUF, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Utalii, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Mazingira, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Benki ya Biashara ya Taifa (NBC), ZSSF, Shirika la Bandari, Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC).

Wengine waliochangia ni Mfanyabiashara wa Zanzibar Bw. Mohammed Raza, Bw. Salum Turkey, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Bw. Haroun Ali Suleiman, Bw. Mohammed Abdallah, Bw. Ahmada Yahya Abdallah, Bw. Amani Ibrahim Makungu,
ambao wote walikabidhiwa vyeti vya shukrani.

No comments:

Post a Comment