27 October 2010

Boakye, Mbegu waishi kwa matumaini Yanga

Na Elizabeth Mayemba

WACHEZAJI wa Yanga, Ernest Boakye na Mohammed Mbegu, wanaendelea kuishi kwa matumaini katika klabu hiyo, huku kila mmoja akisubiri ripoti yake. Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu hiyo,
Louis Sendeu alisema kwa upande wa Boakye, yupo katika matibabu ya tumbo hivyo uongozi unasubiri ripoti ya daktari.

"Boakye siku ya mechi alidai kwamba anasumbuliwa na tumbo la kuhara, hivyo akapewa dawa za kutuliza maumivu na moja kwa moja akarudishwa Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu, kwa sasa tunasubiri ripoti ya daktari na ufafanuzi utatolewa baadae," alisema Sendeu.

Alisema Mbegu, yeye anatuhumiwa kwa utovu wa nidhamu, alipokuwa jijini Tanga wakati timu hiyo ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Azam FC.

Sendeu alisema kutokana na hali hiyo, uongozi wa klabu hiyo umemtimua mchezaji kambini, hadi atakapohojiwa na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.

Alisema utovu wa nidhamu wa Mbegu utatajwa baadaye baada ya kuhojiwa, lakini kwa sasa hawawezi kuweka kosa lake hadharani.

Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti jana kuwa, Mbegu anadaiwa kukutwa na mwanamke chumbani kwake, katika hoteli waliyofikia saa chache kabla ya mpambano wao kuanza.

1 comment:

  1. Huyo Boakye alikuwa garasa na akawa msumbufu pia

    ReplyDelete