27 October 2010

Mgombea mwenza NCCR yuko 'fiti' kwa kampeni

Na Rehema Mohamed

HALI ya Mgombea Mwenza wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. Ally Omary Juma imeanza kutengamaa na sasa amejitokeza wazi na kusema yupo tayari kuendelea na kampeni za chama chake.
Bw. Juma aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali yake hiyo, baada ya kutoonekana hadharani kwa muda, kutokana na kuanguka Oktoba 16, mwaka huu katika Kijiji cha Kivuyu, Jimbo la Micheweni akiwa katika mkutano wa kampeni.

Bw. Juma alisema kwa mujibu wa madaktari waliomtibu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hana tatizo lolote lililobainika ila kilichomsababishia kuanguka ni kukosa hewa kutokana na vumbi alilovuta.

"Baada ya lile tukio nilikuja Dar es Salaam na kwenda hospitali ya Amana kisha Muhimbili ambapo nilipimwa vipimo vyote ikiwemo Ukimwi na sikubainika kuwa na tatizo lolote bali 'aleji' iliyotokana na vumbi nililovuta," alisema Bw. Juma.

Alisema siku ya tukio akiwa jukwaani lilikuja vumbi jingi mfano wa kimbunga, ambalo liliniingia katika mapafu na kufanya nishindwe kupumua vizuri na hatimaye nikaanguka.

Hata hivyo, alisema kuwa madakatari wamemshauri kujiepusha na vumbi ili asipatwe na hali hiyo kwa mara nyingine.

Katika hatua nyingine, Bw. Juma alivitaka vyama vya siasa nchini kuendelea na kampeni kistaarabu ili kuepuka machafuko.

Bw. Juma alisema katika siku chache za kampeni zilizobaki, chama chake kitajikita katika Mkoa wa Dar es Salaam kufanya kampeni kwa kuwa anaamini kuwa ndiko kwenye idadi kubwa ya wananchi.

No comments:

Post a Comment