01 November 2010

Utabiri wa Shekhe Yahya wakwama.

Na Mwandishi Wetu

LICHA ya utabiri wa Mnajimu maarufu nchini, Shekhe Yahya Hussein kubainisha kuwa mwaka huu kusingekuwa na Uchaguzi Mkuu, hali imekuwa tofauti na
uchaguzi huo ukafanyika nchini kote jana, isipokuwa katika majimbo saba, ambako uliahirishwa kutokana na kasoro za karatasi za kura.

Ukiondoa majimbo hayo saba ya Wete, Mwanakwerekwe, Mtoni, Magogoni, Mpanda Vijijini, Mpanda Mjini na Nkenge, maeneo mengine uchaguzi ulifanyika kama ilivyopangwa.

Vyanzo vya habari vilivyozungumza na Majira vilisema kuwa kufanyika kwa uchaguzi huo ni ishara tosha kuwa utabiri huo wa Shekhe Yahya haukuwa kweli.

Februari 4, mwaka huu, gazeti hili lilimkariri Shekhe Yahya Hussein akitabiri kuwa hakutakuwa na uchaguzi mkuu mwaka huu nchini.

Habari hiyo ilitokana na mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Channel Ten katika kipindi cha masaula ya nyota, ambako alionekana akisisitiza utabiri huo mara kwa mara.

Huku akionekana kufafanua utabiri huo, Shekhe Yahya alisema, "nasema hakuna uchaguzi mwaka huu, uchaguzi utaahirishwa, siwezi kusema sana, maana karibuni nilitoa utabiri
kuwa kuna mtu anaweza kufa katika kugombea urais, watu wamesema sana," alisema.

Juhudi za gazeti hili kumpata mnajimu huyo kuzungumzia utabiri wake hazikuzaa matunda, kwa kuwa simu yake ilikuwa ikiita muda wote bila majibu.

Tangu mwishoni mwa mwaka jana Shekhe Yahya alikuwa katikati ya mijadala ya kisiasa nchini, hasa ile inayohusiana na uchaguzi baada ya kutoa utabiri uliopingwa vikali, kuwa mwanachama yeyote ndani ya CCM ambaye angesimama kumpinga Rais Jakaya Kikwete katika nafasi ya urais angekufa ghafla.

Hata hivyo, hakuna mwanachama wa CCM aliyejitokeza kumpinga rais huyo hadi akatangazwa mgombea pekee, baada ya aliyekuwa amesema angempinga, Bw. John Shibuda kuamua kuachia ngazi hata kabla ya kuchukua fomu.

3 comments:

  1. Majini yake hayawezi kushindana na MUNGU aliye hai, waumini wa dini mbalimbali wamesali na Mungu amewasikia. Sasa tatizo lipo kwa Kikwete anayekubali kupokea ulinzi wa majini kutoka kwa Mganga huyo.

    ReplyDelete
  2. Huyu Mzee uzee wake unampeleka kubaya,unajimu wake hauna ukweli, maana hata simba walitaka kumvamia baada ya kuwatabiria watashinda matokeo wakafungwa,Mimi nadhani utabiri wake aliona kuna kifo ikaja taswira jina la Mziray nadhani akahisi ni yule mgombea wa uraisi kumbe kafa kocha duuhh atakufa kifo kibaya cha hasira za watu watamvamia, ni bora akaacha haya mambo ni aibu na si ktk imani za dini.

    ReplyDelete
  3. Huyo mzee anazeeka vibaya, hii siyo mara ya kwanza utabiri wake wa mambo ya uchaguzi mkuu kwenda kapa. Nakumbuka uchaguzi wa 2005 aliwahi kutabiri kuwa wagombea wote wa urais wa uchaguzi wa mwaka 2000 hakuna hata mmmoja atakayegombea 2005.Matokeo yake Lipumba na Mrema waligombea tena 2005.Hii inaonyesha kuwa ni mtoa maoni badala ya mtabiri.Apuuzwe...
    Mathias Mtesigwa-UK

    ReplyDelete