18 August 2010

Yanga, Simba nani atacheka leo

Na Zahoro Mlanzi

BAADA ya tambo, majigambo na kejeli za takribani wiki mbili mfululizo hatimaye sasa mashabiki, wanachama, viongozi, wachezaji na makocha wa timu za Simba na Yanga, leo wanakutana uso kwa uso katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ni mchezo unaovuta hisia kubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini, ambapo mara nyingi timu hizi zinapokutana kwa hakika matukio mengi hutokea kabla na baada ya mechi.

Tukio mojawapo licha ya yale za imani za kishirikina, ambayo wakati mwingine hutokea uwanjani kabla ya mechi kuanza, pia baada ya mechi timu itakayofungwa hutafuta mchawi na mfano mzuri kwa beki Amir Maftah, ambaye alifukuzwa Yanga kutokana na tuhuma za kuihujumu ilipofungwa bao 1-0.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Aprili 18, mwaka huu kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara katika mchezo ambao, Simba ilitoka mbele kwa mabao 4-3. Simba pia ilishinda bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Oktoba 31, mwaka jana.

Mchezo huo hautahusisha vita ya Makocha Wakuu pekee, Patrick Phiri wa Simba na Kostadin Papic wa Yanga, bali hata kwa viongozi na wachezaji, kitu kinachofanya mchezo huo kuvuta hisia zaidi.

Kwa upande wa makocha, Phiri atataka kuendeleza uteja kwa Papic kwani tangu Papic aanze kuinoa Yanga msimu uliopita akichukua mikoba ya Dusan Kondic aliifunga Simba mara moja katika michuano ya Tusker, hivyo naye atataka kuifunga na kuanza kutengeneza rekodi nzuri.

Wakizungumzia mchezo huo kwa nyakati tofauti, makocha hao kila mmoja alitamba kuibuka na ushindi kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

Phiri alisema kikosi chake hakina mabadiliko makubwa zaidi ya kuongeza wachezaji katika safu ya kiungo, beki na ushambuliaji ambapo amewaongeza Rashid Gumbo, Patrick Ochang, Salum Aziz na Amir Maftah.

Papic naye alisema anajivunia mshambuliaji wake mpya Mghana Keneth Asamoah, kutokana na kiwango alichokionesha katika michezo miwili ya majaribio kwa kufunga mabao manne.

Mbali na vita hiyo, pia mshambuliaji Mussa Hassan 'Mgosi' wa Simba atataka kudhihirisha kwamba hakubahatisha baada ya kuibuka mfungaji bora wa msimu uliopita wa ligi hiyo, hivyo atakuwa na kazi ya ziada kumuonesha makali yake Asamoah.

Si hayo tu, hata kwa viongozi wa klabu hizo ambao hivi karibuni wameingia madarakani, kila mmoja atataka kuanza kibarua chake kwa kumfunga mpinzani wake wa jadi kwani imezoeleka hiyo nayo ni sifa pekee ambayo hujivunia, pindi wanapoondoka madarakani.

Mwenyekiti mpya wa Simba, Ismail Aden Rage pamoja na wa Yanga, Lloyd Nchunga watakuwa na kazi ya ziada, kuhakikisha vikosi vyao vinaibuka na ushindi, ili kujiweka katika hali nzuri miongoni mwa wanachama wao.

Katika tathimini ya miaka mitano iliyopita Simba, imekutana na Yanga mara 11, Simba ikishinda mara sita, Yanga imeshinda mmoja na kutoka sare mara nne, hivyo Simba kuonekana kuwa na rekodi nzuri dhidi ya mpinzani wake.

ends......

No comments:

Post a Comment