18 August 2010
Msekwa: Piga ua CCM itashinda
Na John Daniel
ZIKIWA zimebaki siku tatu kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi Mkuu, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetamba kuwa kitaibuka na ushindi kwa kupewa ridhaa na Watanzania kwa awamu nyingine kwa sababu ya kuwa na mtaji wa wanachama wapato milioni tano na mtandao wa mabalozi wake wa nyumba kumi kumi nchi nzima.
Kimesema kuwa kutokana na wanachama wake kuongozwa na ahadi za utiifu na uaminifu kwa chama, CCM kina kura milioni tano kibindoni tayari kabla hata kampeni hazijaanza.
Hayo yalisemwa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Bw. Pius Msekwa wakati akizungumza na Majira ofisini kwake Dar es Salaam, ambapo alisema kutokana na sababu hizo mbili chama hicho kimeamua kutumia kauli mbiu yake ya 'ushindi ni lazima' kikiamini kuwa hakuna chama kingine kinachoweza kukishinda.
"Sisi tunaenda kwenye uchaguzi tayari tuna mtaji wa wanachama zaidi ya milioni tano, tena idadi hiyo siyo ya kubuni ni takwimu kutoka kwenye madaftari yetu ya orodha ya wanachama na wote wana shahada za kupiga kura, ahadi ya mwana CCM ni kuwa mwaminifu na mtiifu, ni lazima ampigie kura mgombea wa CCM, kwa maana hiyo tunajivunia zaidi ya kura milioni tano tayari.
"Wapinzani wanaosema watashinda wajipime kwanza kwa utaratibu huo huo kama wana mtaji kama huo, hizo kura za jukwaani haziaminiki bila kuwa na mtaji wa wanachama kwanza, ndio maana tunasema ushindi wa kishindo ni lazima,wapo wapenzi wetu wengi nao watatuchagua," alisema Bw. Msekwa.
Alisema mabalozi wa nyumba 10 wa CCM watasaidia kampeni za nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu na kukiongezea ushindi chama hicho badala ya kutegemea kampeni za jukwaani.
Kuhusu wanachama wanaohama na kujiunga na vyama vingine kiongozi huyo alisema wanaofanya hivyo walikuwa 'wanachama abiria na si wanachama halisi' wa chama hicho.
"Hao wanaohama si wanachama halisi, ni wanachama abiria, wakikosa gari la ubunge wanapanda gari yoyote watakayokuta stendi ili kuwafikisha kwenye ubunge, hatutetereki wala kuyumba kwa ajili ya watu kama hao, wanachama halisi wote wamebaki, hizo ni hasira za mkizi," alisema Bw. Msekwa.
Alisema tabia ya baadhi ya watu kukihama chama hicho haijaanza mwaka huu na kwamba hata katika chaguzi za nyuma wapo wana CCM waliofanya hivyo baada ya kutoteuliwa lakini baadaye wakaamua kurejea chama hicho baada ya kubaini maana halisi ya demokrasia.
Aliongeza kuwa wanachama 10 au watano kuondoka, kati ya wanachama zaidi ya milioni tano ni sawa na kuchota ndoo moja ya maji katika Mto Rufiji.
Akijibu swali kuhusu kuagushwa katika kura za maoni kwa mmoja wa vigogo wa CCM Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu Bw. John Malecela kisha NEC kubariki, Bw. Msekwa alisema hawana wasiwasi na hali hiyo kwa kuwa ndio demokrasia ndani ya CCM.
"Mzee Malecela lazima aheshimiwe sana, ni mtiifu na mwaminifu kwa chama, hata safari hii hatetereki na atatusaidia kampeni kama miaka ya nyuma, mwaka 2005 alijaribu kugombea urais akashindwa akabaki mwaminifu, kushindwa ubunge si tatizo kwake," alisema Bw. Msekwa.
Kuhusu utata wa uraia wa Bw. Hussein Bashe, alisema vielelezo vilivyochapishwa na gazeti moja jana (si Majira) si vigeni kwake kwa kuwa walivipitia kuanzia kikao cha Kamati Kuu (CC) na baadaye kwenye NEC mjini Dodoma na kujiridhisha kuwa si raia wa Tanzania.
"Mojawapo ya sifa za kumfanya mtu kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa ni kwamba mmoja wa wazazi wake lazima awe raia wa Tanzania, tuna shaka na vielelezo, hivyo huenda vilitolewa kimakosa maana tuna mashaka na uraia wa mama yake, lakini idara husika itatoa taarifa," alisema Bw. Msekwa.
Akizungumzia uamuzi wa NEC kupitisha baadhi ya majina ya wagombea ubunge wenye kesi mahakamani, huku wengine majina yao yakikatwa Bw. Msekwa alisema utofauti uliopo katika mazingira ya kesi hizo ndiyo uliosababisha maamuzi hayo kufikiwa, kwa kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu bila kumwonea mtu.
"Kesi ya Chenge ni trafic case...ya kugonga na kuua, kesi ya Mramba ni matumizi mabaya ya madaraka, kesi ya Mwakalebela ni ya rushwa, TAKUKURU wamejiridhisha kwamba ana kesi ya kujibu, hatuwezi kumteua mtu kisha akawekewa pingamizi siku ya siku," alisema Bw. Msekwa.
Aliwaomba wana CCM kuwa watulivu wakati huu nchi inapoelekea uchaguzi mkuu na kuwa chachu ya amani na utulivu huku akisisitiza kuvunjwa kwa makambi ya wagombea walioshinda na kushindwa katika kura za maoni.
Aliongeza kuwa CCM kitaheshimu maadili ya uchaguzi na kwamba chama hicho kimetoa agizo kwa wagombea wake wote kuheshimu maadili ya uchaguzi kwa kuwa zimewekwa na kupewa nguvu kwa mujibu wa Sheria.
"Mwaka huu tumejipanga kufanya kampeni kisayansi, baada ya uzinduzi wa kampeni tarehe 21 Jangwani mgombea wetu atatembelea kila Mkoa, kila Wilaya kuomba kura,tayari tumepeleka ratiba yetu Tume ya Taifa ya Uchaguzi,tumepanga seti ya magari ya timu ya kampeni kikanda,"alisema Bw. Msekwa.
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment