18 August 2010

Kova kufuturisha uwanjani baada ya mechi

Na Benjamin Masese

JESHI la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema leo litafuturisha waislamu waliofunga ambao watahudhuria mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga, unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Hayo yalisema Dar es Salaam jana na Kamanda wa kanda hiyo, Suleiman Kova wakati wa uzinduzi wa mradi wa mtandao wa wanawake Tanzania (PTF-Net), kuhusu kukabiliana na ukatili wa kijinsia nchini na sheria zake.

Kova alisema maandalizi ya usalama wa raia na mashabiki katika wa mchezo huo umekamilika, ambao umefanywa kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jeshi la Polisi na Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni.

"Kwa kuwa mchezo huo utamalizika jioni na ikizingatiwa hawa wenzetu waislamu wanatakiwa kufuturu nyumbani kwao, sisi Jeshi la Polisi tumetoa ofa ya kuwagharamia, hivyo baada ya mchezo huo kutakuwa na futari yao pale pale uwanjani, wasihofu waje na familia zao," alisema.

Kova alisema mipango kabambe imeandaliwa pamoja na masharti, ili kukabiliana na mashabiki wakorofi watakaojaribu kwenda kinyume na utaratibu uliowekwa uwanjani hapo.

Alibainisha masharti hayo ni pamoja na kutoruhusiwa shabiki au kiongozi yeyote kuingia ndani ya uwanja huo na chupa au mifuko ya aina yoyote ile.

Alisema haitaruhusiwa mashabiki kuhama sehemu moja kwenda nyingine, pia kutakuwa na ukaguzi getini wa tiketi bandia na vitu vingine ambavyo havihusiani na michezo.

Kova alisema tayari kompyuta ya kisasa, imefungwa kwa kuwekea vifaa maalumu kama kamera, ambayo itaonesha watu wote walio ndani ya uwanja huo, ambayo itapokea ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba ya simu za mkononi 0783034224.

Kamanda huyo alisema mtu yeyoto anaruhusiwa kuandika ujumbe na kuutuma kupitia namba hiyo, kama atafanikiwa kumuona shabiki au mtu yeyote anafanya fujo.

Alisema imekuwa ni kawaida wanapocheza watani hao, kutokea vitendo vya ajabu vinavyofanywa na mashabiki na kutoa mwito kwamba watakaokamatwa na polisi wakijihusisha na vitendo viovu wataadhibiwa kwanza na baadaye kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

ends.....

No comments:

Post a Comment