Na John Daniel, Geita
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amemaliza utata kuhusu ni wapi yatakuwa makao makuu ya Mkoa mpya wa Geita, baada baada aya kutangaza kuwa
yatakuwa mjini Geita, na si Chato iliyokuwa inafikiriwa.
Rais Kikwete alisema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa kampeni mjini Gaita ambapo alisema mkoa huo utaanza kufanya kazi rasmi Januari mwakani.
Mkutano huo ulihudhiriwa na umati mkubwa wa watu, ukiwa ni wa tatu baada ya ule uliofanyika mjini Sengerema na Buchosa huku akiahidi kufufua Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Mwanza Nyanza kwa kukipatia sh. bilioni tano.
Rais Kikwete alisimama katika maeneo ya Kamanga Feri, Kijiji cha Nyamatongo, Kata ya Katunguru, Kijiji cha Gasenyi, Kijiji cha Ruchili, Kijiji cha Bukokwa Kata ya Nyakalilo pamoja na mji mdogo wa Kasamwa kusalimia wananchi.
Akiwasalimia wananchi wa Kijiji cha Kamanga feri alipovuka kutoka Mwanza mjini jana asubuhi, Rais Kikwete alisema licha ya kuahidi kumaliza deni la sh. bilioni tano ya Nyanza ili kuwakomboa wakulima wa mkoa huo pia ataangalia uwezekano wa kujenga barabara ya Kamanga- Nyehunge iliyopo katika Jimbo la Buchosa kwa kiwango cha lami ili kuharakisha maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.
"Hivi sasa tunaendelea na ujenzi wa barabara ya Usagara- Sengerema hadi Geita, mwaka huu barabara hii haipo kwenye ilani yetu, lakini jungu kuu halikosi ukoko nitaangalia uwezekano wa kuijenga katika kiwango cha lami. Hii ni ahadi yangu, niachieni," alisema Rais Kikwete huku ashangiliwa na wananchi.
Katika Mji mdogo wa Nyehunge, Rais Kikwete alisema kutokana na kulakiwa na wananchi wengi kupita kiasi ameongezeka uzito kwa nusu kilo kwa kuwa umati huo unampa matumaini mapya ya kuendelea kuwatumikia zaidi Watanzania katika kipindi kijacho kwa kuwa kama wasingemtaka kuendelea wasingejitokeza na kusimama juani kumsikiliza.
"Sisi wanasiasa ukienda mahali ukapokelewa na umati mkubwa hivi unaongezeka uzito kwa nusu kilo na mimi nimeongezeka nusu kilo, nashukuru sana, lakini nataka niwahakikishie kwamba mkinichagua nitawatumikia kwa nguvu zote kuliko wakati uliopita. Mnayo sababu ya kutuchagua, yale tuliyoahidi tumetekeleza na kama yapo machache tunajibu na tutamalizia katika kipindi kijacho," alisema Rais Kikwete.
Alisema baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa victoria hadi Shinyanga, mradi mkubwa unoafuata katika awamu yake ya pili ni kuimarisha elimu kwa kuzipa walimu wa kutosha, maabara, vifaa vya maabara, vitabu, nyumba za walimu shule zote za sekondari za kata ili kuhakikisha kwamba Tanzania inapiga hatua haraka kwa kuwa elimu ndio ufunguo wa maendeleo la Taifa lolote duniani.
Alisema hivi sasa wakulima wa pamba wataendelea kufaidika na mfumo huo wa kilimo kwanza kwa kuwa serikali inalipa nusu ya bei ya mbegu, pembejeo, mbolea na vifaa vingine huku ikiendelea kusambaza matrekta madogo na kupanua kilimo cha umwagiliaji kwa kiasi kikubwa.
Leo Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Kagera.
No comments:
Post a Comment