18 August 2010

Mume wa waziri afia 'gesti'

Na Raphael Okello, Bunda

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bi. Gaudensia Kabaka amepata pigo baada ya mme wake Bw. John Kabaka (65) kukutwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni mjini Bunda mkoani
Mara.

Tukio hilo lilitokea jana asubuhi ambapo dereva wa marehemu Bw. Steven Zablon alieleza kuwa juzi wakiwa na marehemu walitoka nyumbani kwake katika Kijiji cha Sirari wilayani Tarime kwenda mjini Musoma kwa ajili ya kununua vipuri vya gari lake.

Alisema kuwa baada ya kutoka Musoma Marehemu alimtaka dereva kwenda katika Chuo cha Ualimu kilichopo mjini Bunda na kwamba baada ya kufika chuoni hapo gari hilo liliharibika.

"Baada ya kufika hapa chuoni tuliamua kumpeleka mzee mjini kwa ajili ya kutafuta mahali pa kulala na tulipata sehemu inayoitwa Nyasa...baada ya kula chakula cha jioni alituaga kuwa anakwenda kupumzika na kutuomba tumzimie simu zake zote, jambo ambalo tulilitekeleza," alisema dereva huyo.

Aliongeza kuwa siku iliyofuata ambayo ni jana saa mbili asubuhi alikwenda kwenye nyumba hiyo kumwona, lakini pia kuomba fedha za kununulia vipuri lakini walipofika walijaribu kugonga mlango kwa muda na hakukuwa na majibu yoyote kutoka ndani.

"Tulipoona hivyo mmoja wa mafundi alizunguka nyuma na kusukuma kioo cha dirisha na kuona amelala, hali iliyomshtua na kuamua kutoa taarifa polisi Bunda," alisimulia sereva huyo.

Baada ya polisi kufika walibomoa mlango na kukuta amefariki dunia hivyo hatua iliyofuata ni kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika Hospitali ya DDH ya Wilaya ya Bunda ambako mwili huo umehifadhiwa ukisubiri kusafilishwa kijijini kwake kwa mazishi.

Hata hivyo, habari kutoka kwa ndugu wa marehemu zinadai  kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na kwamba wanaaimini kuwa huenda ndicho
kikawa chanzo cha kifo chake.

Kwa upande wake Bi. Kabaka ambaye alifika mjini Bunda  asubuhi baada ya kupewa taarifa hizo kwa simu, alisema kuwa msiba huo ni pengo kubwa kwake hasa katika kipindi hiki kigumu cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Viongozi waliofika katika tukio hilo na kulipokea kwa masikitiko ni pamoja na Waziri wa kilimo, chakula na
ushirika Bw. Stephen Wasira na katibu wa CCM wilaya ya Bunda Bw. Charles Mangwale.


Polisi wilayani Bunda wamethibtisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ambapo hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na
tukio hilo.

Matukio ya kukutwa kwa watu wakiwa wamefariki katika nyumba za kulala wageni yamekuwa yakitokea mara kwa mara mjini hapo ambapo hivi karibuni mama mmoja alikutwa akiwa amefariki katika nyumba moja ya kulala wageni ya Bariadi mjini Bunda.

No comments:

Post a Comment