Na Edmund Mihale
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kuna dalili za hujuma na ubaguzi katika mchakato wa uchaguzi na kimemwandikia Msajili wa Vyama vya
Siasa kuongeza muda wa kujaza fomu za gharama za uchaguzi.
Katika barua yake kwa msajili, chama hicho kimesema kuwa kinazo taarifa kutoka maeneo mbalimbali kuwa wagombea wa CCM wamepatiwa nakala ya fomu husika na wagombea wa CHADEMA kunyimwa fomu hizo, hali inayoashiria hujuma au ubaguzi katika eneo hilo.
Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba V/HQ/MSJ/04/33 ya Agosti 23, mwaka huu, ambayo Majira linayo nakala yake, CHADEMA walikuwa wakijibu barua ya msajili yenye kumbumkumbu namba DB. 173/205/01/77 ya Julai 10, mwaka huu, ambayo chama hicho kilisema kiliipata Agosti 17, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana juu ya barua hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw. John Mnyika alisema kuwa CHADEMA ina mashaka kuwa imeandikwa tarehe za nyuma kwa kuwa kiutaratibu fomu zisingeweza kuwa zimesambazwa kabla ya kanuni husika kukamilika mwezi Julai.
Alisema kuwa wamemuomba msajili wa vyama aongeze muda kutokana na fomu hizo kutoonekana katika Ofisi za Wakurugenzi na Makatibu Tawala wa Wilaya na Mikoa mbalimbali.
"Tunaomba ofisi yako izingatie kuwa maelekezo hayo yamefika yakiwa yamechelewa karibu kabisa na tarehe ya uteuzi wa wagombea wa Agosti 19, mwaka huu.
"Pia tunasikitika kuiarifu ofisi yako kuwa wasimamizi wa uchaguzi na watendaji wengine wanaohusika na mchakato wa fomu husika katika maeneo mbalimbali ya nchi wameshindwa kutoa fomu husika kwa wagombea kwa maelezo kuwa hawakupatiwa na tume wala ofisi ya msajili.
"Hata hivyo kwa taarifa tulizo nazo kutoka katika maeneo hayo wagombea wa CCM wamepatiwa nakala hizo husika hali inayoashiria hujuma ama ubaguzi katika mchakato huo wa uchaguzi," alisema Bw. Mnyika akiisoma barua hiyo na kuongeza:
"Tunaitaka Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa izingatie kuwa mchakato mzima umecheleweshwa na serikali kutokana na kuchelewa kutolewa kwa kanuni husika na kwa upande mwingine ofisi yako itekeleze wajibu wake wa kusambaza fomu hizo kwa wagombea badala ya kuelekeza suala hilo kufanywa na vyama vya siasa.
"Hivyo tunaiomba ofisi hiyo kusogeza mbele tarehe ya mwisho ama iache kabisa kuweka pingamizi kwa wagombea na kutoa maelekezo mbadala kwa wasimamizi wa uchaguzi, makatibu tawala, vyama vya siasa na wadau wengine ili kuepuka wagombea kuenguliwa kwa mapingamizi," alisema Bw. Mnyika.
Alisema wamekuwa wakipokea simu kutoka kwa wagombea mbalimbali wa chama cha hicho kuwa hadi sasa wameshindwa kujaza fomu hizo kutoka na kuambiwa kuwa fomu hizo hazipo katika vituo hivyo.
Katika kuonesha utata uliopo kuzipata fomu hizo, Bw. Mnyika alisema yeye binafsi alikutana na vikwazo alipozifuatilia, hali aliyodai kuwa inaweza kutumika kukihujumu chama hicho, kama ilivyofanyika katika hatua ya uteuzi, kwani mapingamizi mengi yataongezeka.
Majira lilipowasiliana na Msajili wa Vyama, Bw. John Tendwa alisema kuwa atazungumzia suala hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari leo.
Naye Na Suleiman Abeid kutoka Shinyanga anaripoti kuwa CHADEMA huenda kikampoteza mmoja wa wagombea wake wa kiti cha ubunge katika Jimbo la Maswa Mashariki mkoani Shinyanga, Bw. Sylivester Kasulumbai baada ya kuwekewa pingamizi ikidaiwa aliwahi kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja.
Hali hiyo inatokana na pingamizi lililowekwa na mmoja wa wagombea ubunge katika jimbo hilo, Bw. Robert Masunga anayegombea kwa tiketi ya chama cha UDP.
Msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo hilo la Maswa Mashariki Bi. Elizabeth Kitundu alisema Bw. Masunga anapinga kuteuliwa kwa Bw. Kasulumbai kwa vile aliwahi kuhukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja gerezani au kulipa faini ya sh. 600,000.
Bi. Kitundu alisema, Bw. Kasulumbai alihukumiwa adhabu hiyo mapema mwanzoni mwa mwaka huu na kuamua kulipa faini ya sh. 600,000 na kuepuka kwenda jela baada ya mahakama ya wilaya kumtia hatiani kwa kosa la kutishia kuua kwa maneno.
Hata hivyo, msimamizi huyo alisema Bw. Kasulumbai tayari amekata rufaa kupinga pingamizi hilo ambayo imewasilishwa katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambako itajadiliwa kwa mujibu wa sheria na baadaye uamuzi wa kugombea au kutogombea kwa mgombea huyo utatolewa.
Bw. Kasulumbai mapema mwanzoni mwa mwaka huu alitiwa hatiani na mahakama ya Wilaya ya Maswa kwa kosa la kutishia kuua kwa maneno ambapo ilidaiwa alimtisha Ofisa Tawala wa Wilaya ya Maswa, Bw. Anthony Masili kuwa angemkata kichwa na kukitembeza katika mitaa ya Maswa.
No comments:
Post a Comment