Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umekiri kuzidiwa na deni wanalodaiwa na wachezaji wake watatu iliyowaacha katika usajili wa msimu huu na hivyo kuwaomba kuzungumza upya.
Wachezaji walioachwa na Yanga, ambao wanaidai klabu hiyo ni beki raia wa Malawi Wisdom Ndlovu, Mkenya John Njoroge na Steven Marashi ambaye ni raia wa Tanzanaia.
Akizungumza Dar es Salaam juzi Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako alisema ni kweli wachezaji hao wanadai lakini fedha wanazodai kwa sasa klabu yake haina uwezo wa kuwalipa lakini wamewaomba kuwalipa kiasi cha fedha ambazo zitawasukuma hadi katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo.
"Ni kweli wachezaji hawa wanatudai lakini hata hivyo, tumewaita na kuzngumza nao jinsi ya kuwalipa lakini imeonekana wanataka fedha nyingi ambazo kwa sasa hatuna uwezo wa kuwalipa kama wanavyotaka," alisema Mwalusako.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Luois Sendeu alisema kikosi cha timu hiyo kinaendelea vyema na mazoezi yake ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi, Simba ambao utapigwa Jumatano katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Sendeu alisema wachezaji wapo katika hali nzuri na kila mmoja anaonekana kuwa na ari ya ushindi katika mechi hiyo, ambayo inatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na kila timu kufanya usajili mzuri.
"Kikosi chetu kipo imara kwa ajili ya mechi hii na tunategemea wachezaji wetu watafanya vizuri siku hiyo na ushindi ndiyo kitu cha msingi, kwani kama tukishinda itakuwa ni mwanga mzuri wa kuchukua ubingwa wa Tanzania Bara," alisema Sendeu.
Timu hizo kongwe zitacheza mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ikiwa ni ishara ya ufungizi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo inatarajia kuanza kutimua vumbi Agosti 21, mwaka huu katika viwanja mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment