Na Mwajuma Juma, Zanzibar
CHAMA Cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA), kimesema katu hakitopeleka wachezaji wake kutoka Zanzibar ambao wanatakiwa kujiunga na timu ya Taifa 'Taifa Queens', iliyopiga kambi katika Shule ya Filbat Bayi Mkoani Kibaha.
Timu hiyo inajiandaa na michuano ya netiblo ya Afrika, ambayo inatarajiwa kuchezwa nchini Afrika Kusini, ambapo zaidi ya nchi 20 zitashiriki michuano hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kaimu Katibu Mkuu wa CHANEZA, Rahima Bakari alisema chama chake kimeamua kuchukua uwamuzi huo kutokana na viongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kukwepa kufanya vikao vya pande mbili za Muungano.
Alisema wameamua kutoa tamko hilo, baada ya Kaimu Katibu wa CHANETA, Rose Mkisi kukaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa mgogoro kati ya vyama hivyo, umemalizika na kuwataka wao Zanzibar kupeleka wachezaji kujiunga na kambi hiyo.
Rahima alisema CHANETA na CHANEZA, vilikubaliana katika kikao cha pamoja chini ya usimamizi wa mabaraza ya michezo Tanzania (BMT) na BMZ kuwa mashindano yoyote ya kimataifa, yaandaliwe baada ya viongozi wa vyama hivyo kukaa pamoja.
Alisema mambo ya msingi waliyokubaliana ni mashindano ya kimataifa ni lazima viongozi wote wapange bajeti na utaratibu wa kuwapata wachezaji na si upande mmoja, kuamua kwa niaba ya mwingine.
Katibu huyo alisema katika suala la mikutano ya kimataifa ilikubaliwa kwamba, ujumbe lazima uwe na sura ya Muungano, jambo ambalo limekuwa halizingaitiwi na Mwenyekiti wa CHANETA hicho.
"Na mfano ni Mei 15, mwaka huu Mwenyekiti wa CHANETA, Anna Bayi alihudhuria mkutano wa Afrika Kusini, kinyume na maazimio yaliyofikiwa Aprili 27 Nairobi, Kenya.
“CHANEZA bado inasisitiza haitopeleka wachezaji kujiunga na timu ya taifa na hiyo ni kutokana na Mwenyekiti wa CHANETA, kujiamulia mambo yote peke yake, tumechoka kuburuzwa Tanzania maana yake Zanzibar na Tanganyika,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo CHANEZA imeamua mwaka huu, haitoshiriki ligi ya Muungano na timu iliyoweka kambi katika Shule ya Filbat Bayi ni ya Tanzania Bara na si ya Muungano.
Msimamo huo wa CHANEZA, umekuja baada ya Rose kuitaka CHANETA kupeleka wachezaji wakajiunge na kambi kabla ya mashindano hayo ya Afrika kufanyika.
Mashindano hayo ndiyo yatakayotoa timu tatu, zitakazoiwakilisha Afrika katika mashindano ya Kombe la Dunia ya netiboli yatakayofanyika nchini Singapore.
No comments:
Post a Comment