Na Esther Macha,
Rungwe
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imewahukumu
kunyongwa hadi kufa watu wawili waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji dhidi
ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja.
Watuhumiwa hao wawili ni
kati ya watuhumiwa wanne waliokuwa wakikabiliwa na kesi hiyo.
Hukumu hiyo ilitolewa jana
katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, iliyokuwa ikiendesha vikao vyake katika
Mahakama ya Wilaya ya Rungwe chini ya Jaji Samweli Karua.
Awali kabla ya kusomwa kwa
hukumu hiyo mwendesha mashtaka wa Serikali, Archiles Mulisa, aliwataja
watuhumiwa wanne kuwa ni Hakimu Mwakalinga, Daudi Mwasipasa, Obote Mwanyingili
na Kelvin Myovela ambao wanatuhumiwa kumuua kwa makusudi aliyekuwa Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja.
Alisema watuhumiwa hao
waliokuwa wakikabiliwa na kesi namba 131/2012 walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika Kijiji cha
Mpandapanda, Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Mulisa aliyekuwa
akisaidiwa na Wakili wa Serikali Lugano Mwakilasa kwa upande wa mashtaka huku
watuhumiwa wakitetewa na mawakili wawili ambao ni Victor Mkumbe na Simon
Mwakolo.
Alisema katika kutetea
hoja zao upande wa mashtaka ulileta mashahidi 11 ambao wote kwa pamoja
wakiongozwa na shahidi namba moja waliwatuhumu washtakiwa kuhusika na tukio hilo.
Jaji Karua alisema pamoja
na ushauri wa wazee wa baraza la mahakama ambao pia wanawatuhumu washtakiwa hao
kuhusika na tukio hilo
naye alikubaliana nao lakini siyo kwa watuhumiwa wote.
Waliohukumiwa kunyongwa
hadi kufa ni Hakimu Mwakalinga na Daudi Mwasipasa, huku wengine wakihukumiwa
adhabu ya kwenda jela miaka saba. Mtuhumiwa huyo ni Mwanyingili ambaye
alipatikana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa aliyehusika kufanya mauaji hayo.
Kwa upande wa mtuhumiwa
Myovela alitiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika katika mauaji
hayo ingawa hakuhusika na kitendo hicho moja kwa moja.
Alisema
kutokana kosa hilo
mtuhumiwa huyo atatumikia kifungo jela miaka saba ingawa pia tayari alikuwa amehukumiwa
kifungo jela cha miaka 20 kwa kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment