14 November 2013

MJAMZITO AUAWA KWA KUCHINJWA Na Faida Muyomba, Geita
  Mwanamke mjamzito mkazi wa kijiji cha Nyamalembo wilayani Geita, Magdalena Kyaruzi (26) , ameuawa kikatili nyumbani kwake kwa kukatwa panga shingoni na mtu anayesadikiwa kuwa mgeni.

Mwanamke huyo alikuwa na ujauzito wa miezi minne, ambapo mumewe ni mfanyakazi wa kampuni ya Moolman, inayojishugulisha na uchimbaji dhahabu katika mgodi wa Geita (GGM).
Kamanda wa Polisi mkoani Geita , Leonard Paulo , alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. "Ni kweli tukio hili lipo na lilitokea juzi saa 3:30 asubuhi, ambapo mtu ambaye hadi sasa hajulikani jina wala sura yake alifika nyumbani kwa mama huyu kisha kufanya ukatili huo wakati mumewe akiwa kazini,"alisema.
  Alisema muuaji huyo kabla hajafanya ukatili huo, alifika nyumbani hapo na kubisha hodi alipokaribishwa ndipo alianza kumkata mapanga sehemu ya kisogoni, kichwani na kufa papo hapo.
Alisema, mara baada ya kutimiza azma yake hiyo, muuaji huyo alitoweka na simu ya marehemu, na kuwa taarifa za kiintelijensia zinaeleza kuwa mtu huyo aliwahi kufika nyumbani hapo mwezi mmoja uliopita.
"Uchunguzi wetu wa awali umebaini kuwa mwezi mmoja uliopita wakati mumewe akiwa hayupo, alifika hapo na kufanya mazungumzo naye jambo linaloonesha kuwa walikuwa wanafahamiana," alisema.
   Alisema, jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi zaidi kubaini chanzo chake na kwamba hakuna mtuhumiwa anayeshikiliwa kutokana na mauaji hayo.

No comments:

Post a Comment