14 November 2013

SIMBA: TUTAFANYA USAJILI KIMYAKIMYA



 Na Elizabeth Mayemba
  Uongozi wa klabu ya Simba umesema kuwa usajili wake katika kipindi hiki cha dirisha dogo watafanya kimyakimya kwa ajili ya kukwepa hujuma, kwani kuna klabu zinasubiri klabu hiyo itangaze nia ya kusajili mchezaji fulani ili wavuruge.

Akizungumza na gazeti hili jana mmoja wa wajumbe wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini, alisema watamtangaza mchezaji pale tu watakapoingia naye mkataba.
"Sisi hatusajili kwa kutangaza nia, tutakapomhitaji mchezaji fulani tutakubaliana naye na kuingia naye mkataba ndipo tutakapomtangaza rasmi katika vyombo vya habari," alisema Mjumbe huyo.
Alisema kuna klabu zinasubiri kuona Simba inamnyatia mchezaji gani ili nao waingilie kati, lakini kwa staili hiyo safari hii hawawapati na badala yake watasikia tu washamsainisha mchezaji wanayemtaka.
  Mjumbe huyo alisema timu yao inamapungufu katika kila idara, hivyo watatafuta wachezaji ambao wataondoa tatizo hilo kwa lengo la timu yao kutwaa ubingwa msimu huu tofauti na watu wanavyofikiria.
  Alisema kuwa inashangaza kuona baadhi ya watendaji ndani ya Simba wanathubutu kusema kuwa Simba haichukui ubingwa, hali ambayo inaonesha ni kuwakatisha wachezaji tamaa na wakati nafasi waliyonayo wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo.
  Kiongozi huyo alisema kwa sasa mengi yatasemwa kuhusu timu yao, lakini wao wanaamini kwamba ubingwa watauchukua na wale wanaotamba mapema kabla ya mzunguko wa pili haujaanza wataishia kuumbuka.
  Simba wamemaliza ligi hiyo wakiwa na pointi 24 na kushika nafasi ya nne, huku vinara wa ligi hiyo wakiwa Yanga wenye pointi 28 ikifuatia Azam FC wenye pointi 27 sawa na Mbeya City

No comments:

Post a Comment