28 November 2013

TIMU ZA CHINA, VIETNAM KUCHEZA ZANZIBAR



 Na Mwajuma Juma, Zanzibar
 Timu za soka za Vietnam na Jamhuri ya Watu wa China, zimetumiwa mialiko na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Mapinduzi yatakayofanyika Zanzibar mwezi ujao
.
  Timu hizo zimealikwa, ili kupamba sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yanayofikia kilele chake Januari 12 mwakani.
  Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kupitia mwandishi wake, Othman Khamis ilieleza kuwa mwaliko huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa Balozi Seif Ali Iddi, alipokuwa akizungumza na Mabalozi wa nchi za Vietnam na Jamhuri ya Watu wa China kwa nyakati tofauti.
  Balozi Seif alisema Serikali tayari imeshaandika barua kwa nchi hizo na hatua hiyo, imefikiwa kutokana na msimamo wa nchi hizo kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara baada ya kupata uhuru mwaka 1964.
  Taarifa hiyo ilieleza kuwa Serikali imejiandaa kuzihudumia timu hizo kwa kutoa huduma za malazi, chakula na usafiri wa ndani wakati zitakapokuwa nchini, huku nchi hizo zikitakiwa ziwapatie tiketi za usafiri wa kwenda na kurudi Zanzibar.
  Kwa upande wao mabalozi hao, Nguyen Thanh Nam wa Vietnam na Lu youqing wa China wakizungumza na Balozi, Seif wameahidi kulishughulikia ipasavyo suala hilo la mualiko, ili kuona kwamba lengo lililokusudiwa la kutoa mwaliko huo linafanikiwa vyema.
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu yatakuwa na makundi matatu, mawili yatakuwa yakicheza Uwanja wa Amaan na kundi moja litacheza Uwanja wa Gombani, Pemba.

No comments:

Post a Comment