13 November 2013

JK ARUDISHA ZAWADI YA DHAHABU



 Rais Jakaya Kikwete, amerudisha zawadi ya dhahabu safi gramu 227 aliyopewa na Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya mkoani Geita na kutaka itumike kuwasaidia watoto yatima, anaripoti Mwandishi Wetu
. Zawadi hiyo alikabidhiwa juzi katika sherehe ya uzinduzi wa Mgodi wa Uchenjuaj iDhahabu wa kampuni hiyo uliopo nje kidogo ya Mji mdogo wa Kharuma ambako ndiko Makao Makuu ya Wilaya Mpya  ya Nyang’hwale,mkoani humo.
  Dhahabu hiyo ina thamani ya sh. milioni 16 kwa bei ya sasa katika soko la dhahabu duniani ambapo baada ya kukabidhiwa, Rais Kikwete aliuliza; “Sasa nifanye nini na zawadi hii, naomba kuirudisha hii dhahabu muiuze popote, fedha ambayo itapatikana tutawapa watoto yatima,” alisema.
  Akizungumza na wananchi katika mgodi huo, Rais Kikwete aliupongeza uongozi wa mgodi na kusema umeongeza thamani ya dhahabu na ya maisha ya wananchi katika eneo hilo.Aliushauri uongozi wa mgodi huo, kufanya jitihada za kuboresha teknolojia inayotumika. “Mgodi huu ni mradi wa maana sana kwani umeongeza thamani ya dhahabu na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili, ubunifu huu unastahili pongezi.
  “Lazima tuboreshe teknolojia, ile inayotumika katika mgodi huu ni ya zamani kidogo, hii ni sawa na hadithi ya mtu mwenye chongo katika jamii ya vipofu watupu, yeye anaonekana kama mfalme,” alisema Rais Kikwete.
  Mgodi wa Nyamigogo ni wa marudio kwa maana ya kuzalisha dhahabu kutokana na mchanga ambao awali ulifukuliwa ili kutoa dhahabu na ulianzishwa mwaka 2011 ambapo hadi sasa, sh. bilioni 1.6 zimewekezwa katika uendelezaji wa mgodi huo.
  Katika risala ya uongozi wa mgodi huo, ilisema mgodi huo unazalisha kati ya gramu 500 na 600 kwa mwezi na umeajiri watu 45 wakiwemo wanawake 10.Tangu kuanzishwa kwake, umekuwa unaunga mkono shughuli za jamii inayouzunguka kwa kujenga zahanati na madarasa ya shule katika vijiji viwili.
  Rais Kikwete amezindua mgodi huo kama sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo akiwa katika ziara yake rasmi ya kikazi mkoani humo ambao ni miongoni mwa mikoa minne aliyoianzisha mwaka 2012.
  Ziara hiyo imemalizika jana kwa kupokea ripoti ya maendeleo ya Wilaya ya Nyang’hwale na kuhutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mji Mdogo wa Kharuma

1 comment:

  1. Mimi sitashangaa iwapo vigogo wengine watakuwa wamepokea zawadi kama hii bila ya kutangaza.

    ReplyDelete