13 November 2013

DKT. MVUNGI AFARIKI DUNIA

  • ALIKUWA KWENYE MATIBABU AFRIKA KUSINI
  • NCCR- MAGEUZI KUZUNGUMZIA MSIBA LEO 
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi, amefariki dunia jana alasiri nchini Afrika Kusini, katika Hospitali ya Milpark, Johannesburg.

Dkt. Mvungi ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi na Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB), alipelekwa nchini humo baada ya kuvamiwa na kujeruhiwa usiku wa kuamkia Novemba 3 mwwaka huu akiwa nyumbani kwake, Kimbamba Msakuzi.
Chama cha NCCR-Mageuzi, kimethibitisha juu ya kifo hicho na kuongeza kuwa, taarifa kamili zitatolewa leo Makao Makuu ya chama yaliyopo Ilala, kuanzia saa tatu asubuhi.
Mtoa habari hizo ndani ya chama ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema marehemu Dkt. Mvungi alikuwa kiongozi mkubwa ndani ya chama na ametumia fursa hiyo kukifanya chama hicho kiwe na wanachama wengi.
Dkt. Mvungi baada ya kujeruhiwa kwa mapanga, alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Tumbi, iliyopo Kibaha, mkoani Pwani na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
Kutokana na hali yake kutoimarika vizuri akiwa hospitalini hapo, Novemba 7 mwaka huu, Dkt. Mvungi alisafirishwa kwa ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Flightlink, kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi hadi mauti yalipomkuta wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake.
Msemaji wa Kitengo cha Taasisi ya Mifupa (MOI), Bw. Jumaa Almas, alisema walilazimika kumsafirisha Dkt. Mvungi kutokana na afya yake kutoimarika vizuri.
Dkt. Mvungi alipata majeraha makubwa kichwani ambapio katika msafara wake, aliongozana na Daktari Bingwa wa Upasuaji Ubongo na Mishipa ya Fahamu Dkt. Clement Mugisha na Muuguzi, Bi. Juliana Moshi.
Juzi Jeshi la Polisi nchini kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alisema watu tisa ambao walihusika kumpiga, kumjeruhi na kuiba vitu mbalimbali vya marehemu Dkt. Mvungi, tayari wamekamatwa.
Dkt. Nchimbi alisema watu hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa nyakati tofauti ambapo awali walikamatwa sita na juzi kufikia tisa.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, ambaye alikuwepo katika mkutano huo, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Msigwa Mpopela (30), Shabago Magozi na Hamadi Ally, jina maarufu 'Hatibu'.
Wengine ni Zakaria Raphael (dereva wa bodaboda), Mmanda Saluwa, Juma Hamisi, Longisho Semeriko (muuza ugolo), Paul Jeirosi na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Kilimimazoka, ambao wote ni wakazi wa Dar es Salaam
"Watuhumiwa hawa walikutwa na mapanga, kigoda ambavyo vimethibitika kuwa vilitumika katika tukio hilo, pia walikutwa na simu ya mkononi mali ya Dkt. Mvungi," alisema.
Kamishna Kova alisema, katika mahojiano ya awali na watuhumiwa, walikiri kuhusika na tukio hilo na ushahidi umekamilika kwa asilimia 80.
"Watuhumiwa wote wamekiri kosa hivyo tunakamilisha upelelezi ili wafikishwe mahakamani mara moja," alisema.
Marehemu Dkt. Mvungi, aliwahi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi



2 comments:

  1. What a loss in the academia. Rest in peace beloved

    ReplyDelete
  2. I remember him and Dr. Tenga during a research work in Manyara and Arusha regions on pastoralism and policy discourses

    Your legacy is irrefutable in the academia!

    ReplyDelete