24 October 2013

VODACOM YAWAPAMBA WAHARIRI Na Goodluck Hongo
  Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, jana imekabidhi vifaa mbalimbali vya michezo kwa timu ya wahariri wa vyombo vya habari na timu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 3.5.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalimu alisema wameamua kutoa vifaa hivyo kutokana na umuhimu wa vyombo vya habari kwa umma.
  Alisema licha ya Vodacom kudhamini Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini pia wanaendelea kudhamini mashindano mengine hivyo kwa mechi ya wahariri na waandishi wa habari ni muhimu kutokana na wahariri wengi kukosa nafasi hata ya kucheza mpira.
 “Tumekutana na wahariri mara tatu na walipoomba udhamini kwetu sisi tulikubali na kuamua kutoa vifaa hivi kama jezi, viatu, mipira na suti za michezo ambapo licha ya vifaa hivyo lakini mshindi katika mechi hiyo atapata jezi,” alisema Mwalimu.
   Naye nahodha wa timu ya jukwaa la wahariri, Kulwa Karedia ambaye ni Mhariri wa gazeti la Mtanzania alisema wanaishukuru kampuni hiyo kwa mchango wao wa kutoa vifaa hivyo, ili kufanikisha mechi hiyo ya aina yake ambayo itachezwa Jumamosi mkoani Iringa.
  Alisema wao wamejiandaa vizuri kwa kuishinda timu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa (Iringa Press Club) kwa kuwa wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo, baada ya kufanya mkutano wao na Kampuni ya Vodacom uliofanyika mkoani humo.
  “Tunaishukuru mno Vodacom kwa msaada huu walioutoa, ili kufanikisha mechi yetu hasa sisi watu wa habari, lakini kama wahariri tumejiandaa vizuri katika mechi hiyo na tutashinda,” alisema Karedia.

No comments:

Post a Comment