11 October 2013

MGOMO WASAFIRISHAJI :PINDA: MALORI, MABASI RUKSA

  •  AMTAKA MAGUFULI,WADAU KUFIKIA MWAFAKA
  • ARUDISHA MSAMAHA WA ASILIMIA TANO MIZANI
Na Darlin Said
 Waziri Mkuu , Bw. Mizengo Pinda , amesitisha utekelezwaji wa agizo la Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli la kuondoa msamaha wa tozo kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubalika kisheria.

Bw. Pinda alitoa uamuzi huo Dar es Salaam jana siku moja baada ya Chama cha Wamiliki wa Malori nchini (TATOA), kutangaza uamuzi wa kupaki magari yao wakipinga agizo hilo.
TATOA pamoja na Chama wa Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (TABOA), walipinga agizo la Dkt. Magufuli kutaka magari yanayobeba uzito wa tani tatu na nusu na kuendelea, kupimwa mizani bila msamaha wa tozo uliozidi ndani ya asilimia tano ya uzito uliokubaliwa kisheria.
Alisema kutokana na sakata hilo, amelazimika kuunda kamati ambayo itakutana na wadau TATOA na TABOA ili kupata ufumbuzi wa mgogoro uliojitokeza.
"Kwa kuwa bado kuna mgogoro kati ya Wizara ya Ujenzi, Wasafirishaji wa malori na mabasi kuhusu utekelezwaji wa kanuni 7(3), ambao wanasema haitekelezeki kirahisi, naiagiza Wizara ikutane na wadau. "Wakae na kujadili namna bora ya kutekeleza kanuni hii, Wizara ya Ujenzi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, waunde timu ya wataalamu ambao watakutana na wawakilishi wachache wa TATOA na TABOA ili wapitie kanuni hizi kwa lengo la kupata mwafaka," alisema Bw. Pinda.
Aliongeza kuwa, mwezi mmoja unatosha kwa Wizara na wadau hao, kukamilisha kazi hiyo na utaratibu uliokuwepo awali kabla ya tangazo la Serikali uendelee kutumika.
Aliitaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kupanga utaratibu mzuri wa kupima magari hayo katika mizani ili kuondoa msongamano katika kituo kimoja.
"Wakati umefika kwa Wizara husika kukagua mizani na kuangalia ubora wake kwani hicho ndio chanzo kikuu cha mgogoro uliopo... baadhi ya watumishi katika mizani si waaminifu, wanapokea rushwa hivyo Wizara iangalie namna ya kutatua tatizo hili," alisema.
Akizungumzia  barua iliyoandikwa mwaka 2006 na Waziri wa Miundombinu (wakati huo), Bw. Basil Mramba. Barua hiyo ilitoa nafuu ya punguzo la asilimia tano ya uzito wa 'Axel' za magari utakaosomwa kwenye mizani ili kufidia kasoro za mizani kutopima kwa usahihi uzito wa magari.
   Alisema msamaha huo ulikuwa kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani, sura ya 168, toleo la 2002 na kanuni zake za mwaka 2001 za Usalama Barabarani juu ya ukomo wa uzito wa magari.
  "Ingawa Bw. Mramba alifanya hivyo kwa nia njema, wasafirishaji wakatumia fursa hiyo vibaya kwa kuongeza mizigo kwenye magari yao kwa sababu kuna msamaha wa asilimia tano," alisema.
  Bw. Pinda alisema, kutokana na hali hiyo Dkt. Magufuli aliamua kufuta muongozo wa barua hiyo na kujielekeza katika sheria na kanuni za Usalama Barabarani za mwaka 2001.
  Sheria hiyo inasema uzito uliozidi lakini upo ndani ya asilimia tano ya uzito unakubalika kisheria, magari hayo yanapaswa kupunguza mzigo, kupanga mzigo na ikishindikana watatakiwa kulipia uzito mara nne ya tozo ya kawaida.
  Awali Bw. Pinda alisema, Serikali haitaruhusu malori na mabasi kuzidisha mizigo kama nafuu wanayoitafuta kwani barabara zilizopo zina uwezo wa kudumu miaka 20 kwa magari yaliyobeba uzito unaokubalika kisheria. mzia mgogoro huo, Bw. Pinda alisema chanzo chake ni baada ya Dkt. Magufuli kufuta

No comments:

Post a Comment