02 October 2013

PONDA AKWAA KISIKI MORO



 Na Ramadhan Libenanga,Morogoro

 Kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Morogoro, jana imeahirishwa baada ya wakili wake, Bw. Juma Nassoro, kuwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu katika kipindi cha mwezi mmoja.


Shekhe Ponda alifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo wakili Bw. Yahaya Njama ambaye akimwakilisha mahakamani hapo, aliiambia mahakama hiyo kuwa, Bw. Nassoro anasumbuliwa na macho.

"Mheshimiwa Hakimu(Richard Kabate),nimekuja hapa mahakamani kumwakilisha wakili wa mshtakiwa (Nassoro), ambaye anasumbuliwa na macho hivyo yupo safarini nchini India kwa matibabu ya mwezi mmoja," alisema Bw.Njama.Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo,Bw .Kabate alisema kutokana na udhuru ya Bw. Nassoro, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 7, mwaka huu.

  Wakili wa Serikali, Bw. Bernard Kongola,aliuomba upande wa mshtakiw a kuhakikisha Bw. Nassoro anafika mahakamani siku hiyo ili kesi hiyo ianze kusikilizwa na kupunguza gharama za Serikali kuendesha kesi kutokana na kumsafirisha mshtakiwa kila inaposomwa katika mahakama hiyo.

   Shekhe Ponda anakabiliwa na mashtaka matatu ambapo Agosti 10 mwaka huu, eneo la Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Morogoro, anadaiwa kuwaambia Waislamu wasikubali uundwaji wa Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti akidai zimeundwa na Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA), ambao ni vibaraka wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali.

  Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwaagiza waumini hao kuwa, kama watu hao watajitokeza kwao na kujitambulisha ni Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha wawapige.Ilielezwa kuwa, kauli hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu  Mkazi Kisutu, iliyotolewa na Hakimu Victoria Nongwa, Mei 9 mwaka huu, iliyomtaka ahubiri amani kwa mwaka mmoja.

  Shtaka la pili, ilidaiwa Agosti 10 mwaka huu, eneo la Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Morogoro, Shekhe Ponda aliwaambia Waislamu Serikali ilipeleka jeshi mkoani Mtwara kushughulikia vurugu zilizotokana na gesi ili kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wananchi ni Waislamu.

  Shekhe Ponda anadaiwa kuwaambia wafuasi wake kuwa Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wananchi wa huko ni Wakristo.

  Shtaka la tatu ambalo linafanana na lile la pili, nalo linadaiwa kutendwa Agosti 10 mwaka huu, ikidaiwa Shekhe Ponda aliumiza imani za watu wengine kinyume na kifungu cha sheria namba 390 na kanuni ya adhabu namba 35 cha mwaka 2002, lakini aliyakana mashtaka hayo.

No comments:

Post a Comment