02 October 2013

OBAMA AFUNGA SERIKALI MAREKANI



WASHINGTON, Marekani
Nchi ya Marekani imelazimika kufunga baadhi ya shughuli za Serikali kuanzia jana, baada ya Bunge la nchi hiyo kuikataa bajeti yake wakipinga mabadiliko ya kisheria yanayohusu sekta ya afya yaliyofanyika hivi karibuni.

Idadi kubwa ya watumishi wa Serikali watakosa ajira ambapo idara nyingi za Serikali zimeambiwa zifunge milango wakati matumaini ya suluhisho la mtafaruku huo wa bajeti ambao unahusisha wabunge wa chama tawala cha Democrat dhidi ya Republicans yakizidi kufifia.
Wataalamu mbalimbali nchini humo walidai kuwa, uamuzi wa kusitisha huduma zisizo muhimu, utaathiri uchumi wa nchi hiyo kwa kiwango kikubwa.Wafanyakazi katika vitengo mbalimbali vya Serikali, jana alfajiri walijikuta wakirudishwa majumbani karibu 800,000 kati yao wakiambiwa wachukue likizo bila malipo hadi mwafaka utakapopatikana.
Marekani imesema wafanyakazi ambao watabakizwa kazini ni wale ambao shughuli zao haziwezi kusimama kama madaktari, manesi, waongoza ndege na wafanyakazi wa Shirika la Posta nchini humo.Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW), ilisema baadhi ya huduma za umma kama miradi ya utafiti wa tiba zinazoendeshwa na idara za Serikali zitasimama.
NASA ambacho ni kitengo kinachofanya tathmini za usafiri wa kwenda sayari nyingine na anga za mbali, wafanyakazi asilimia 95 wamepewa likizo bila malipo katika kipindi hiki.Marekani imefikia hatua hiyo baada ya Baraza la Seneti linalodhibitiwa na Chama cha Democrat kukataa pendekezo la wajumbe wa Chama cha Republican la kuusimamisha mpango wa huduma za afya wa Rais Obama ujulikanao kama Obama Care.
  Wabunge wa Republican wanaolidhibiti Baraza la Wawakilishi, walikuwa tayari kuipitisha bajeti hiyo kwa sharti la kuusimamisha mpango wa afya wa Obama ambao umeanza kutekelezwa jana.Kutokana na kufungwa kwa shughuli za Serikali, Rais Barack Obama wa nchi hiyo alisema; "Kwa bahati mbaya Bunge halikutimiza wajibu wake".
  Rais Obama aliwatumia wanajeshi ujumbe wa video akisema; "Kama amiri jeshi wenu, nimehakikisha kwamba mtaendelea kuwa na uwezo, zana na yote mnayoyahitaji ili kuutekeleza wajibu wenu kwa Taifa."Vitisho kwa Taifa letu, bado havijabadilika hivyo tunawataka muwe tayari kwa dharura yoyote," alisema Rais Obama na kuwashukuru askari wa kujitolea na wale wa Idara ya Ulinzi kwa huduma zao."
  Kila upande unaulaumu mwingine kushindwa kufikia makubaliano ambapo Rais Obama amehadharisha madhara ya kiuchumi yanayoweza kutokea kutokana na kusimamishwa shughuli za Serikali akisema kasi ya ustawi wa uchumi inaweza kuvurugika.
  Hatua iliyofikiwa jana pia imesababisha wasiwasi kama Marekani itafikia lengo lake hadi katikati ya Oktoba mwaka huu la kuongeza deni la Serikali hadi dola trilioni 16.7.
  Hisa barani Ulaya zimepanda mapema jana ambapo wawekezaji vitega uchumi wameingiwa wasiwasi. Wachunguzi wanaamini kuwa, wabunge wa Marekani watakaa chini haraka ili kutafuta ufumbuzi.
Wakati huo huo, uchunguzi wa maoni umeonesha Chama cha Republican kitalaumiwa na wananchi wengi wa Marekani kutokana na kufungwa kwa shughuli za Serikali.

No comments:

Post a Comment