02 October 2013

MBUNGE LEMA AFUTIWA SHTAKA



Na Jane Edward, Arusha
   Kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema (CHADEMA), imefutwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini humo
  Uamuzi wa kuifuta kesi hiyo ulitolewa na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Bi. Devotha Msofe, baada ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Elianenyi Njiro, kuieleza mahakama hiyo kuwa hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Bw. Njiro alisema; "Mheshimiwa Hakimu, hatuna nia ya kuendelea na kesi hii hivyo tunaiondoa mahakamani kwa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama kilivyorekebishwa mwaka 2002," alisema.
Hakimu Msofe aliridhia uamuzi huo na kumuachia huru Bw.Lema chini ya kifungu hicho cha Sheria ya Makosa ya Jinai.Wakili wa pande zote waliridhika na uamuzi huo wa mahakama kumuachia huru Bw. Lema ambaye alikuwa nje kwa dhamana.
Akizungumza na Majira nje ya mahakama , Bw. Lema alisema alikuwa akijua kesi hiyo ya kutengenezwa ndiyo maana mashahidi walikuwa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya.Alisema kwa kuwa kesi hiyo imefutwa kwa kifungu kidogo cha sheria, hataogopa kusema ukweli na kuachiwa kwake kutamfanya ashirikiane na wapigakura kuharakisha maendeleo yao.

No comments:

Post a Comment