23 October 2013

MALINZI KUANIKA MIKAKATI YAKE LEO


Na Mwandishi Wetu
  Zikiwa zimebaki siku nne kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mgombea wa nafasi ya urais, Jamal Malinzi leo anatarajiwa kukutana na waandishi wa habari kuzindua rasmi kampeni zake, huku akitoa mpango endelevu wa kuendeleza soka nchini ndani ya kipindi chake.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaam jana, Malinzi alisema ameamua kuzindua rasmi kampeni zake ili Watanzania wajue kile ambacho anakusudia kukifanya, iwapo atachaguliwa kuongoza chombo hicho.

"Kwangu ni muhimu zaidi Watanzania wajue sera zangu na wafahamu nini nitafanya iwapo nitashika madaraka ya kuiongoza TFF.

"Unaweza ukawa shahidi jinsi ambavyo Watanzania wengi wanavyopenda soka, lakini imetokea bahati mbaya soka haiwapendi wao. Kuna mahali tunatakiwa kurekebisha, hicho ndicho kitu ninachotaka kuweka hadharani.

"Huu si wakati wa kupiga kelele, lazima tuangalie tulipokosea na tuchukue hatua za haraka kurekebisha, sitaki kuweka kila kitu hadharani, ni vyema kesho (leo) tuisubiri na utajua kila kitu kuhusu mimi.

 "Naamini nitaeleweka kwa Watanzania na wapiga kura ndani ya TFF, kesho (leo) si mbali ila ni kusubiri na kujua kile ambacho nitakitoa kwenu," alisema.

Malinzi, mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kutwaa kiti hicho kutokana na uwezo wake mkubwa wa uongozi ndani ya vyama na klabu za michezo hapa nchini, alisema pamoja na yote hayo anaamini hakutakuwa na mchezo mchafu katika uchaguzi huo.

 "Tuache mtu anayetakiwa ndiye aongoze chombo hicho, kwangu ninachotaka ni haki na kutokuwepo kwa mchezo wowote mchafu," alisema.

  Uchaguzi Mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo, ambapo unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka hapa nchini kujua nani atatwaa kiti hicho kutoka kwa Leodegar Tenga.

  Malinzi alifanikiwa kupita katika kuwania nafasi hiyo, baada ya zengwe kubwa kuibuka kwake huku awali jina lake liking'olewa kabla ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kutaka uchaguzi uahirishwe ili kusikiliza malalamiko ya wagombea mbalimbali.

  Mwongozo wa FIFA ndiyo uliosaidia kwa kiasi kikubwa kwa Malinzi kurejea kugombea nafasi ya urais ndani ya TFF.

No comments:

Post a Comment