24 October 2013

MALINZI AAHIDI NEEMA AKIWA RAIS TFFNa Mwandishi Wetu
  Mgombea Urais katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema endapo atachaguliwa katika nafasi hiyo, anaahidi kuenzi mafanikio ya awamu inayomaliza muda wake.

  Akizungumza Dar es Salaam jana, Malinzi alisema moja ya mafanikio hayo ni kustawisha utulivu katika uendeshaji wa mpira na kufanya jitihada za kubuni, kuboresha na kustawisha maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
  “Jitihada kubwa zitawekwa kwenye muundo wa idara ya ufundi, katiba ya TFF imeainisha kuwa shirikisho hilo ndiyo msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, hivyo jukumu la kuleta maendeleo ya mchezo huu kwa kiasi kikubwa linaiangukia TFF.
  “Kwa msingi huu, basi asilimia kubwa ya rasilimali za TFF lazima ziwekewe katika kuleta maendeleo ya mpira. Kwa mfumo wetu wa uendeshaji, kichocheo kikuu cha maendeleo ya mpira ni idara ya ufundi TFF,” alisema Malinzi.
  Alisema pia msisitizo uwepo kwenye ujenzi wa kituo cha mpira (Football Centre of Excellency), ni kituo maalumu cha mafunzo ya mpira wa miguu, ambapo katika kituo hicho kuna kila aina ya miundombinu, viwanja vya kufundishia mpira, vituo vya tiba, madarasa, maabara za utafiti, hosteli na vinginevyo.
  Malinzi alisema kuhusiana na suala la timu kupanda daraja, ili kuongeza ushindani na kupanua mpira uchezwe kona zote nchini, mtindo wa kucheza kikanda ili kupata timu za kupanda daraja kuu utakuwa ni wa kudumu na utaimarishwa kwa kutafutiwa udhamini na kuboreshwa viwanja kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanja hivyo.
 “Kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya zamani, wataalamu wa kandanda wanasema kuwa ili mchezaji awe katika kiwango bora inabidi acheze kwa mwaka kimashindano wastani wa mechi 40. Ligi yetu kuu inatoa fursa kwa mchezaji kucheza michezo 26 kwa mwaka iwapo atapangwa kila mechi hiyo haitoshi,” alisema.
  Kwa upande wa mpira wa wanawake, Malinzi alisema hadi sasa hakuna mfumo imara na unaoeleweka wa kuendeleza soka la akinamama, ambapo alisema soka hilo la wanawake lilianzia Wilaya ya Kinondoni na kukulia huko ambapo kuna timu zenye majina kama Mburahati Queens na Sayari Queens.
  Pia alisema maandalizi ya vijana ni lazima mpango endelevu wa maendeleo ya soka la vijana uandaliwe mapema, uratibiwe na kusimamiwa kwa makini.“Ndugu zangu nasisitiza kuwa maendeleo ya mpira Tanzania kwa hapa yalipofikia yanahitaji ubunifu, ujasiri na msukumo mpya ili tuweze kuunyanyua mpira wetu na kuupa mwelekeo mpya, mwelekeo wa matumaini, mwelekeo wa kulipeleka soka letu katika kushinda vikombe vikubwa barani mwetu Afrika na duniani,” alisema.

No comments:

Post a Comment