09 October 2013

JK ATULIZA WAPINZANIMwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba (katika), akizungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, Dar es Salaam jana, kuhusu vyama hivyo kusitisha maandamano ya kupinga rais kusaini rasimu ya Muswada wa Katiba Mpya. Kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
  •  WASITISHA MAANDAMANO,WAKUBALI MEZA YA MAZUNGUMZO
  • JUKWAA LA KATIBA LAWAPA WOSIA,LATAKA WAWE NGANGARI

 Na Mariam Mziwanda
   Vyama vitatu vya siasa vinavyoshirikiana katika muungano wa kushinikiza k utokusaini wa kwa Muswaada wa Katiba vimeridhia kukutana na Rais Jakaya Kikwete, pamoja na kusitisha maandamano yaliyopangwa kufanyika nchi nzima kesho.

 Wakati viongozi hao wakifikia uamuzi huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, ametaka viongozi wa vyama hivyo watakapoenda kuonana na Rais Kikwete, kutokuwa wepesi na ahadi watakazoahidiwa na kiongozi huyo wa nchi badala yake wawe ngangari kusimamia hoja za msingi.
Kauli hiyo ya Kibamba inatokana na viongozi wa vyama hivyo vya CUF, NCCR-Mageuzi na CHADEMA kutangaza kuwa wapo tayari kukutana na Rais Kikwete, walipozungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.
Mkutano wa viongozi hao ulifanyika Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi, ambapo Mwenyekiti wa viongozi hao, Prof Ibrahim Lipumba, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na taarifa walizopata kupitia vyombo vya habari kuwa Rais Kikwete, yupo tayari kukutana nao wameona ni busara kuahirisha michakato ya kisiasa.
Prof. Lipumba alisema Rais Kikwete ameonesha busara ya kuhitaji mazungumzo. ”Tumepata taarifa kupitia vyombo vya habari na mitandao na tumekubali kuwa tayari endapo Rais anahitaji mazungumzo, basi tuzungumze naye hivyo tunatoa taarifa kwa umma kuwa tunasitisha maandamano ambayo maandalizi yake yalikuwa yamekamilika ambayo yalikuwa yaanze Oktoba 10 (kesho) hadi tutakapokutana na Rais,” alisema.
  Aliongeza kuwa wakiwa wanasubiri mazungumzo hayo na Rais Kikwete ambayo yatajadili mustakabali wa Katiba Mpya, kupitia Umoja wao wanamshauri Rais Kikwete kuwa ni busara asisaini Muswada huo ili kuondoa kasoro zilizopo na kufanya majadiliano.
  Walisifu muda ambao Rais Kikwete amepanga kukutana nao ambao ni kati ya Oktoba 13 na 15. "Huu ni muda mwafaka katika kupata mchakato wa Katiba Mpya unaoheshimu matakwa ya wananchi na muungano wa nchi mbili kutokana na umuhimu wa jambo hilo," alisema.
  Akizungumza kwa kina hatua hiyo ya vyama vya upinzani, Kibamba alisema kuwa katika mazungumzo ya awali kati ya ofisi yake na viongozi hao, Jukwaa lilishauri juu ya umuhimu wa kukutana na Rais Kikwete iwapo nafasi hiyo ingetokea.
  "Tuliwaambia wasiichezee kwani itakuwa mwafaka badala ya maandamano ambayo yanatumia nguvu nyingi," alisema na kuongeza;
"Nawasihi viongozi hao kutokuwa laini (wepesi) sana kwenye ahadi watakazopewa na Rais badala yake kuwepo na makubaliano yenye hoja za msingi na yanayotekelezeka kwa mahitaji ya Rais..hivyo ni lazima wawe ngangari," alisema.
  Aliongeza kuwa wananchi waelewe wanasiasa wanaangalia zaidi sanduku la kura na hoja zao huwa hazifikirii wananchi waliopo vijijini hivyo viongozi hao ni muhimu kutambua suala hilo.
“Hivyo nasisitiza wasije kutoka Ikulu na makubaliano ya wingi wa nafasi za uongozi bungeni badala ya masilahi ya Watanzania wote," alisema Kibamba.

2 comments:

  1. Replies
    1. JK warudishe bungeni wakagaragazwe tena kwa kura. Hawana majority!!!

      Delete