23 October 2013

BILAL AONGOZA KUAGWA NYAISANGA


  • PADRI ATAKA WAANDISHI WA HABARI WAHESHIMIWE

  Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili wa aliyekuwa mtangazaji mkongwe na Meneja wa Kituo cha Abood Media, marehemu Julias Nyaisanga, aliyefariki dunia Oktoba 20 mwaka huu, mkoani Morogoro, baada ya kusumbuliwa na kisukari. Marehemu Nyaisanga aliagwa jana katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni Dar es Salaam
 Na Rehema Maigala

  Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, jana ameongoza mamia ya wananchi kuaga mwili wa aliyekuwa mtangazaji mkongwe na Meneja wa Kituo cha Abood Media, marehemu Julias Nyaisanga, aliyefariki dunia Oktoba 20 mwaka huu, mkoani Morogoro.


  Marehemu Nyaisanga aliagwa katika viwanja cha Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika Tarime, mkoani Mara.

  Akizungumza katika viwanja hivyo, Dkt. Bilal alisema marehemu Nyaisanga alikuwa kipenzi cha watu, mtangazaji ambaye ametumia taaluma yake kuelimisha jamii hivyo ni vyema waandishi wa habari wakafuata nyayo zake.

  Aliongeza kuwa, marehemu alifanya kazi yake katika mazingira magumu kwani kipindi alichoanza kazi, kulikuwa hakuna vyombo vingi vya habari kama ilivyo sasa.

  Naye Padri Stephano Kaombwe wa Kanisa Katoliki ambaye ndiye aliyeongoza ibada, alisema tangu enzi za mababu hakuna mwanahabari duniani anayekumbukwa kwa mazuri ambayo ameyafanya japo wao ndiyo chumvi katika jamii.

 “Bila ya kuwa na wanahabari ni sawa na chakula kisicho na chumvi, wanahabari wanatusaidia kutuelimisha, kufundisha hata kuburudisha hivyo tunapaswa kuwaheshimu,” alisema.

   Aliongeza wanahabari wanapaswa kuiheshimu chumvi ambayo wameipata kutoka kwa Mungu ili kuikomboa dunia hii.Marehemu Nyaisanga aliwahi kufanya kazi Radio Tanzania, Dar es Salaam (RTD) kwa sasa TBC Taifa na Kampuni ya IPP Media, akiwa Mkurugenzi wa Radio One.

  Viongozi mbalimbali wa vyama, Serikali, taasisi, wamiliki wa vyombo vya habari, Jukwaa la Wahariri waliungana kumuaga marehemu Nyaisanga ambaye ameacha mke na watoto watatu. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.

No comments:

Post a Comment