- YALIA KUHUJUMIWA MECHI YA J'MOSI
Na Hamis Miraji, Mbeya
UONGOZI wa Klabu ya Yanga, jana
umewasilisha barua yao ya rufaa katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), ikitaka mechi dhidi ya Mbeya City irudiwe kutokana na kufanyiwa hujuma
.Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania
Bara, iliyochezwa Jumamosi Uwanja wa Sokoine jijini hapa timu hizo zilitoka
sare ya bao 1-1.
Kabla ya mechi hiyo kuchezwa mashabiki
wanaodhaniwa wa Mbeya City walivamia basi lililobeba wachezaji wa Yanga na
kusababisha kuvunjika kioo cha basi hilo.
Akizungumza jijini hapa jana Ofisa
Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema timu yake ilifanyiwa vurugu na
kusababisha wachezaji kucheza kwa woga, kitu ambacho kimesababisha wacheze
chini ya kiwango na kutoka sare hiyo.
"Wachezaji walitoka kwenye mchezo
kwa kufikiria kufanyiwa vurugu na kushindwa kufanya kile walichotakiwa jambo
lililowafanya kutoka sare ya bao 1-1," alisema Kizuguto.
Alisema licha ya kushambuliwa ndani ya
uwanja, hata walivyotoka uwanjani baada ya mechi kumalizika mashabiki wa Mbeya
City waliendelea kushambulia gari la viongozi wa Yanga aina ya Noah.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Mbeya
City umeiomba radhi Yanga kwa vurugu zilizotokea katika mechi hiyo iliyokuwa na
upinzani mkubwa.
Akizungumza jijini hapa jana Katibu
Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema wanaiomba radhi Yanga kwa matatizo
yaliyojitokeza katika mechi hiyo.
"Sisi kama viongozi tunaomba radhi
kwa wenzetu wa Yanga kwa yaliyotokea siku ya mchezo wetu wa Ligi Kuu,"
alisema Kimbe.
Kimbe alisema kitendo kilichofanyika si
cha kiungwana, hivyo wanakemea kwa nguvu zote.
Alisema wamewapa majukumu vyombo vya dola kwa atakayebainika
atachukuliwa hatua kali za kisheria
No comments:
Post a Comment