02 September 2013

WAZIRI MULUGO AWAPA CHANGAMOTO WATANZANIANa Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutumia teknolojia ya elimu masafa na mitandao kwa kupata taarifa za uhakika za kitaaluma na kimaendeleo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Vodacom Elimu Expo 2013 juzi, jijini Dar es Salaam, Waziri Mulugo alisisitiza kuwa ushiriki wa wandau wote kuendeleza sekta ya elimu unafungua fursa ya kupata na kutoa elimu bora kwa kila Mtanzania.
Maonesho ya Vodacom Elimu Expo 2013 ni ya kwanza nchini Tanzania ambapo yamedhaminiwa na kampuni ya simu ya Vodacom kupitia huduma yake ya M-Pesa.Waziri Mulungo alisema: "Hii ni fursa kubwa kwa wote wanaoshiriki maonesho haya hususan wanafunzi, walimu na wazazi.
Yanatoa nafasi kwa kila mdau wa elimu kuchangia maendeleo ya elimu nchini."Alisisitiza kuwa Serikali kupitia wizara ya elimu, ipo katika hatua za mwisho za kutengeneza mkongo wa taifa utakaounganisha upatikanaji wa mtandao nchi nzima kapitia programu ijulikanayo kama 'Tanzania Beyond Tomorrow' kwa kushirikiana na kampuni za mawasiliano katika kuboresha elimu ya masafa.
"Naipongeza kampuni ya Vodacom kwa kuwa kampuni ya kwanza nchini kushirikiana na Serikali kutekeleza mpango ili kuhakikisha kuwa sekta ya elimu inaendelea na kuwa bora zaidi," alisema.Naye Robert Mihalo, ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Green Acres ya jijini alipongeza wadhamini na waandaaji wa maonesho hayo akisema:
"Nimeweza kubandilishana mawazo na wanafunzi wa shule zingine. Zaidi ya yote, nimepata mbinu mpya kwa kupanua wigo wa ushiriki wa wanafunzi katika kuleta elimu bora Tanzania."Naye Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Vodacom, Kelvin Twissa, ambao ni wadhamini wakuu wa maonesho hayo alionyesha matumaini yake kwa maonesho hayo na kusema kampuni yake inaelewa umuhimu wa elimu kwa kila mtoto kwa hiyo wanajisikia fahari kudhamini maonesho hayo kwani yanalenga kuboresha elimu ya Tanzania. Maonesho hayo yamemalizika jana.

No comments:

Post a Comment