02 September 2013

TARIME WALILIA HAKI ZA WANAUME



 Na Timothy Itembe, Tarime
.WANANCHI wa Kata ya Mriba Tarafa ya Ingwe wilayani Tarime mkoani Mara wamesema katiba mpya ijayo itamke wazi haki za wanaume ili kuwalinda na unyanyasaji ambao unafanywa na wanawake kwenye ndoa. 

Wakitoa maoni wananchi hao siku ya kukusanya maoni iliyoandaliwa na Chama cha Wakulima na Wafugaji (CHAWAWATA) walisema kuwa kuna haja katiba ijayo itamke wazi haki za wanaume asilimia 50 kwa 50 ili kuwalinda na unyanysaji ambao unafanywa na wanawake wao wa ndoa.
Akizungumza Diwani Mstaafu kata ya Mriba, Abdi Gasaya alisema kuwa baada ya wanawake kupewa haki wametumia nafasi hiyo vibaya na kuwanyanyasa wanaume ikiwa ni pamoja na kuwanyima tendo la ndoa kwa madai kuwa wamebakwa.
Mkazi wa Kijiji cha Mangucha, Philipo Wambura alisema kuwa kutokana na wanawake kuwanyanyasa wanaume kuna haja katiba ijayo itamke wazi haki za wanaume na kuwalinda dhidi ya unyanyasaji uliopo kama vile kuwanyima chakula wakidai kuwa nenda ukale uliko kuwa.
Aidha, wananchi hao waliongeza kusema kuwa wanaunga mkono Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba kupendekeza Tanzania kuwa na Serikali 3 Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia waliongeza kusema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika zitajitegemea kiuchumi aidha uchumi utawezesha kila serikali kustawi bila kutegemea serikali nyingine

No comments:

Post a Comment