07 September 2013

TANZANIA KUADHIMISHA SIKU YA UTALII DUNIANI

Na Eckland Mwaffisi
TANZANIA inatarajia kuadhimisha Siku ya Utalii duniani, kuanzia Septemba 23 hadi 29 mwaka huu, ambayo kitaifa itafanyika Jijini Mwanza.Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, imesema Siku ya Utalii Duniani huadhimishwa Septemba 27 kila mwaka
."Siku hii inaratibiwa na Wizara hii, uongozi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na wadau wa tasnia ya utalii nchini...nchi zote wanachama wa Shirika la Utalii Duniani, husherehekea siku hii ambayo kimataifa, inaadhimishwa katika Visiwa vya Maldives," ilifafanua taarifa hiyo.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaaka huu inasema "Utalii na Maji-Kulinda Hatima Yetu, ambapo kwa kuzingatia kauli hiyo, wadau wote wanaombwa kushiriki ipasavyo.Wadau hao ni pamoja na sekta za uhifadhi wa mazingira, maji, wafanyabiashara wa tasnia ya utalii na maliasili, taasisi za elimu, wanasiasa, viongozi na wataalamu mbalimbali.
Shughuli ambazo zitafanyika katika maadhimisho hayo ni pamoja na mashindano ya uandishi wa insha mbalimbali juu ya mada, burudani mbalimbali, maonesho ya utalii, malikale, misitu na masuala ya uhifadhi, teknolojia mbalimbali na ziara ya kutembelea Hifadhi ya Saanane.Taarifa hiyo imeongeza kuwa, utalii ni nyenzo ya kuhamasisha uhifadhi kwa uhai na ustawi wa Taifa.

No comments:

Post a Comment