- AWATAKA WAPINZANI KUTAMBUA DHAMANA YAO
- CHADEMA,CUF WAINGIA BUNGENI WAONDOKA
Mariam
Mziwanda na Rehema Maigala
WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, jana
aliahirisha Mkutano wa Bunge la 12, mjini Dodoma,
ambalo lilipitisha Miswada mitatu ukiwemo wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji wa
mwaka 2013.Miswada mingine ni
Muswada wa Sheria wa Vyama vya Ushirika wa Mwaka 2013 na Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013.
Katika hotuba yake,
Bw. Pinda aliwaomba wabunge kutoka upinzani watambue umuhimu wa chombo hicho na
kutambua dhamana waliyopewa na Watanzania wanaowawakilisha.Alisema wabunge hao wanapaswa kutumia busara na kuona umuhimu wa
kushiriki vikao vya maamuzi kwa masilahi ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia
vita dhidi ya dawa za kulevya nchini, alisema mapambano hayo hayawezi
kukomeshwa na nchi moja hivyo yatafanikiwa kama nchi zote duniani zitaungana
ili kudhibiti biashara hiyo kwani wauzaji, wasafirishaji na watumiaji wanaishi
kwenye jamii na baadhi yao
wanafahamika.
“Nitoe wito kwa
wananchi wote, kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwafichua na kutoa
taarifa za watu ambao wanajihusisha na biashara hii... Serikali itaendelea
kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika,” alisema Bw. Pinda.
Ujenzi miundombinu ya gesi
Bw. Pinda
alisema, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kitaifa ya kipaumbele
katika sekta ya Nishati kupitia Mfumo Mpya wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo
Makubwa’ (Big Results Now).
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka
Mtwara-Lindi hadi Dar es Salaam
na kujenga mitambo miwili ya kusafisha gesi hiyo katika maeneo ya
Mnazi Bay-Madimba (Mtwara) na Kisiwa cha Songo Songo (Lindi).
Hadi sasa meli nne kati ya
12, zimewasili nchini zikiwa na shehena ya vipande 16,623 vya mabomba ambayo
yameanza kusambazwa katika maeneo husika ambayo yatawezesha ujenzi wa bomba wa
umbali wa kilomita 194 kati ya kilomita 532.Aliongeza kuwa, ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa
mradi unaendelea ambapo kazi ya kulaza bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
inategemewa kukamilika Juni 2014 na mradi wote utakamilika Desemba 2014.
Bomba hilo la gesi
linatarajiwa kusambaza gesi katika maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa, Somanga
Fungu, Mkuranga, Dar es Salaam na maeneo mengine
ya Tanzania
kwa matumizi mbalimbali.Baada ya kipindi cha maswali na majibu, alisimama
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Angellah Kairuki kuwasilisha hoja za
Serikali kuhusu muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ya Mwaka 2013.
Kabla Bi. Kairuki hajaanza kuzungumza, wabunge wa
upinzani kutoka vyama vya CHADEMA na CUF walisusia kikao cha Bunge na kutoka
nje ya ukumbi huo.
Kitendo hicho kilisababisha baadhi ya wabunge
kuomba mwongozo juu ya vurugu zilizotokea bungeni juzi ambapo Mbunge wa
Simanjiro, mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, akihoji msamaha wa kiti cha
Spika kwa wabunge waliohusika na vurugu hizo.Alisema kitendo cha Mbunge wa Mbeya mjini, Bw. Joseph
Mbilinyi (CHADEMA), kuchukua sheria mkononi na kumpiga askari wa Bunge ni cha
fedheha.
No comments:
Post a Comment