19 September 2013

SIMBA YAFANYA MAUAJI TAIFA



  •  YANGA YABANWA MBAVU TENA

Na Elizabeth Mayemba
TIMU ya Simba, jana ilifanya mauaji baada ya kuwafunga Mgambo Shooting mabao 6-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Katika mechi hiyo, Simba ilianza kusherehekea bao lake la kwanza kwa dakika ya nne lililofungwa na Amis Tambwe kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi safi iliyochongwa na beki Idrisa Rashid ‘Baba Ubaya’.

Dakika ya 12 mshambuliaji wa Simba, Tambwe alikosabao baada ya kuubabatiza mpira uliokuwa unaokolewa na mabeki wa Mgambo Shooting, lakini shuti lake likatoka nje ya lango.Betram Mombeki wa Simba alikosa bao dakika ya 30 baada ya kuunasa mpira na kuachia shuti kali lililotoka nje ya lango.Simba ilipata bao la pili dakika ya 32 kupitia kwa Haroun Chanongo, ambaye alifunga bao hilo baada ya kipa kutoka ndani ya lango lake na kuupachika mpira kiulaini.
Tambwe aliendelea kuwaumiza Mgambo Shooting, baada ya kuifungia Simba bao la tatu dakika ya 41 baada ya kuunasa mpira uliotemwa na kipa wa Mgambo, Kulwa Manzi ambaye alitema shuti kali la Chanongo.Dakika ya 44 Tambwe aliipatia tena Simba bao la nne ikiwa ni bao lake la tatu katika mechi hiyo, baada ya kuunganisha krosi ya Amri Kiemba.
Simba ilitawala mpira kwa kiasi kikubwa huku kipa wa Simba, Abel Dhaira kuwa likizo Mgambo walizinduka dakika ya 45 na kufanya shambulizi la nguvu, ambapo nusura ingepata bao lakini Novat Lufunga akiwa nje ya 18 aliachia shuti kali lililopaa juu ya lango.Kipindi cha pili Mgambo waliingia kwa nguvu na kuliandama lango la Simba ambapo dakika ya 58, Salum Kipanga alikosa bao la wazi baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa Dhaira na mpira kuwahiwa na mabeki walioutoa nje ya uwanja.
Dakika ya 64, Simba ilipata bao la tano baada ya beki wa Mgambo Bakari Mtama kujifunga akimalizia shuti lililopigwa na Chonongo akiwa katika harakati za kuokoa mpira.Hamis Tambwe aliipatia Simba bao la sita dakika ya 18 kwa mkwaju wa penati baada ya beki wa Mgambo kuunawa mpira akiwa katika eneo la hatari.
Naye Hamis Miraji anaripoti kutoka Mbeya kuwa, katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Sokoine Yanga ilibanwa mbavu na Prisons baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1Mechi hiyo ilianza kwa timu zote kukamiana ambapo dakika ya nane, Simon Msuva nusura aifungie Yanga bao baada ya kuachia shuti kali lililotoka nje kidogo ya lango akiwa nje ya 18.
Dakika ya 19 Six Ally wa Prisons akiwa nje ya 18 naye aliachia shuti kali ambalo hata hivyo lilitoka nje ya lango.Jerry Tegete aliipatia Yanga bao dakika ya 41 kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi ya Mbuyu Twite.Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kuingia na uchu wa mabao ambapo dakika ya 70, Didier Kavumbagu alipiga shuti lililotoka nje ya lango.Prisons ilisawazisha bao hilo dakika ya 78 kupitia kwa Ibrahim Isaka, baada ya kuunganisha kona iliyochongwa na Omega Seme.
Naye Speciroza Joseph anaripoti kuwa Azam FC imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Ashanti katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex Chamanzi, Dar es Salaam.
Kutoka Uwanja wa Mabatini, Chalinze Omari Mngindo anaripoti kuwa Ruvu Shooting imetoka kifua mbele kwa kuwafunga ndugu zao JKT Ruvu bao 1-0.Nako katika Uwanja wa Manungu, Morogoro wenyeji Mtibwa Sugar imelazimishwa suluhu na Mbeya City

No comments:

Post a Comment