Na Mwandishi Wetu
WAKATI homa ya shindano la Redd's Miss
Tanzania ikiwa inapanda kwa washiriki wote, mrembo Prisca Clement juzi usiku
amefanikiwa kutwaa taji la Redd's Miss Tanzania Talent lililofanyika katika
hoteli ya Giraffe iliyopo Kunduchi, Dar es Salaam.
Kutokana na
ushindi huo, Prisca ambaye anatokea Sinza akiwakilisha Kanda ya Kinondoni,
amefanikiwa kuingia katika hatua ya 15 Bora ya Redd's Miss Tanzania.
Majaji wa
shindano hilo walilazimika kumpa ushindi Prisca kutokana na uhodari wake wa kucheza
na moto, hivyo kuwashinda washiriki wote 30 wa shindano hilo.
Watazamaji wengi waliofurika katika
ukumbi wa hoteli hiyo, walikubaliana na uamuzi wa majaji wa kumpa ushindi huo.
Shindano la Redd's Miss Tanzania
linatarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Mlimani City, uliopo
Mwenge, Dar es Salaam ambapo mshindi ataondoka na gari dogo lenye thamani ya sh
milioni 15 na kitita taslimu cha fedha cha sh. milioni 8.
Mbali na mshindi kutwaa zawadi hizo,
mshindi wa pili atapata sh. milioni 6.2, mshindi wa tatu sh. milioni 4, mshindi
wa nne sh. milioni 3, mshindi wa tano sh. milioni 2, mshindi wa sita hadi 15
atapata sh. milioni 1.2 na waliobaki watapata sh. 700,000 kila mmoja.
Akizungumzia ushindi huo, Prisca
alisema hiyo ni dalili njema kwake ya kutwaa taji hilo na ana uhakika mkubwa
atafanikiwa kuwa mshindi.
Naye Meneja wa Redd's Original,
Victoria Kimaro alisema, shindano la mwaka huu limekuwa na msisimko mkubwa
zaidi kutokana na washiriki wote kuwa na sifa zinazolingana.
"Mwaka huu Redd's Miss Tanzania
imepata washiriki bomba zaidi na naamini litakuwa na ushindani mkubwa na wa
aina yake," alisema Victoria.
Taji la Redd's Miss Tanzania kwa sasa
linashikiliwa na Brigitte Alfred aliyelitwaa taji hilo mwaka jana na kukabidhiwa
gari aina ya Noah pamoja na kitita cha sh. milioni 8.
Shindano la Redd's Miss Tanzania linadhaminiwa na Kampuni ya Bia
Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd's Original.
No comments:
Post a Comment