Na Suleiman Abeid, Kahama
SERIKALI imedhamiria
kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ili kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi
unaotoa ajira kwa vijana na kuongeza pato la mwaka kwa wananchi tofauti na
sasa.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyasema hayo juzi, wakati
akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa vijiji mbalimbali vilivyopo Wilaya
za Kahama, Mkoa wa Shinyanga na Bukombe mkoani Geita alipokuwa katika ziara ya
kukagua utekelezaji wa mradi wa upelekaji umeme vijijini (REA).
Alisema
kipaumbele cha Wizara hiyo kwa sasa ni kuhakikisha nchi inapata umeme wa
uhakika ambao utatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na matumizi
ya nishati ya gesi ili kuleta mapinduzi kwenye sekta ya viwanda.
Aliwataka
wakazi wa vijijini wenye tabia ya kwenda mahakamani ili kudai walipwe fidia ya
nguzo za umeme kupita katika mashamba yao waache mara moja kwani inachelewesha
utekelezaji wa mradi huo mkubwa wenye lengo la kuwakomboa katika umaskini.
"Serikali
imedhamiria kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi katika sekta ya nishati ya
umeme kupitia kauli mbiu ya uchumi na maendeleo, juhudi hizi zitafanikiwa kama
Watanzania wenyewe tutaunga mkono jambo hili.
"Tunataka
ifikapo 2015, kuwepo ongezeko kubwa la Watanzania wanaotumia umeme angalau
asilimia 30, Shirika la Umeme nchini (TANESCO), limejipanga kuhakikisha
tunafikia lengo la kuzalisha megawati 3,000 ambazo tutaweza kuuza nje ya nchi
na kuiwezesha nchi yetu kutekeleza miradi yake mingi ya maendeleo,"
alisema.
Prof. Muhongo aliwahadharisha mawakala waliopewa kazi ya
kusambaza umeme vijijini, kuhakikisha wanafanya kazi hiyo kwa kuzingatia muda
uliomo katika mikataba na wakala ambaye atazembea, ataondolewa na kupewa
mwingine.
No comments:
Post a Comment