Na Charles
Mwakipesile, Mbeya
SERIKALI imetangaza kufuta vibali vya
wanaofanya kazi ya kuingiza kemikali nchini kwa ajili ya kudhibiti matumizi
yake ikiwemo tindikali ambayo imekuwa ikitumika kwa ajili ya uhalifu na
kutishia maisha ya Watanzania.
Mkemia Mkuu wa
Serikali, Prof. Samwel Manyele alitangaza uamuzi huyo jana wakati akizungumza
na Dawati la Mkoa la Ukatili wa Kijinsia katika ofisi ya Mganga Mkuu mkoani
Mbeya.
Alisema kuwa,
Serikali imekuwa ikipambana na uingizaji holela wa kemikali ambao ndiyo umekuwa
chanzo cha kubadili matumizi ya kemikali ambazo zimekuwa zikitumika ovyo katika
machimbo na wahalifu ambao wamekuwa wakitumia kwa ajili ya kuangamiza maisha ya
Watanzania.
"Tatizo kubwa
tulilolipata ni kutokana na waingizaji, wasafirishaji, watumiaji kubadili
matumizi ya kemikali na kuishia kuzifanya ni sehemu ya silaha za kuangamiza
Watanzania, hali ambayo sisi kama wadhibiti hatuwezi kukubali iendelee, sasa
tumefuta vibali vyote na wanaotaka wataomba upya ili tuweze kupata nafasi ya
kuwabaini wanaopotosha matumizi," alisema.
Hata hivyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Agnes Buto alisema
kuwa ujio wa Mkemia Mkuu unatoa majibu ya maswali mengi waliyokuwa nayo
kuhusiana na utendaji wa ofisi hiyo ambayo imekuwa ni muhimu sana kwa kazi zao
wakati wote.
No comments:
Post a Comment