23 September 2013

MAJANGA YAIKUTA YANGA SC TAIFA



  •  AZAM FC 'YAINYUNYIZIA LAMBALAMBA'

 Na Elizabeth Mayemba

   Azam FC jana waliifunga Yanga mabao 3-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
   Mpira ulianza kwa kasi ambapo Azam walipata bao la kwanza dakika ya kwanza lililowekwa kimiani na John Bocco kwa kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na Brian Umony.

Azam walifuata tena lango la Yanga dakika ya tano, Humphrey Mieno akiwa na kipa Ally Mustafa 'Berthez' alipiga shuti lililotoka nje ya lango. 
Yanga ilizinduka dakika ya tisa ambapo, Didier Kavumbagu alipata nafasi nzuri ya kufunga lakini shuti lake likatoka nje ya lango.

  Dakika ya kumi, Jerry Tegete aliachia shuti kali lililogonga mwamba na kurudi uwanjani ambapo mabeki wa Azam wakaokoa.

  Yanga waliendelea kulibana lango la Azam na kulitia kashikashi ambapo dakika ya 12, Mbuyu Twite alipiga shuti kali mpira wa faulo lakini kipa akapangua na kumkuta Kavumbagu alipiga nje ya lango.

  Twite nusura angeipatia Yanga bao dakika ya 43, baada ya kuachia shuti kali akiwa nje ya 18 lakini mpira ukagonga mwamba na kutoka nje.

  Yanga waliibana Azam kwa kiasi kikubwa na kuwafanya kurudi nyuma kulinda lango lao na kuwapa nafasi wapinzani wao kufanya mashambulizi kila mara.

Kipindi cha pili dakika ya 49, Kavumbagu aliipatia Yanga bao baada ya kupewa pasi ndefu na Haruna Niyonzima na kuukwamisha mpira wavuni.

Dakika ya 59, Hamis Kiiza aliyechukua nafasi ya Tegete akiwa na kipa, alipiga shuti kali lililookolewa na kipa.

Kiiza alirekebisha makosa yake dakika ya 65 baada ya kuipatia Yanga bao la pili baada ya kupokea pasi ya Simon Msuva.

Dakika ya 69, Kipre Tchetche aliisawazishia Azam bao la pili kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Yanga Kelvin Yondan kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Azam ilipata bao la tatu dakika ya 90 kupitia kwa Joseph Kimwaga baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Tchetche.

No comments:

Post a Comment