22 September 2013

KIVUMBI


Wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa vya upinzani, wakinyoosha mikono ikiwa ni ishara ya kukubaliana na matamko ya viongozi wa vyama hivyo, wakati wa mkutano wa kupinga kupitishwa kwa mswada wa Katiba Mpya katika mkutano uliofanyika kwenyeViwanja vya Jangwani Dar es Salaam jana.


  • Wapinzani wampa JK mtihani ndani ya wiki mbili
  • Askofu Kakobe nae amtaka asisaini mswada
  • Maandamano nchi nzima yanukia iwapo utapita
 Anneth Kagenda na Salim Nyomolelo

   Viongozi wa Vyama vya Siasa vya upinzani wamempa Rais Jakaya Kikwete, muda wa wiki mbili na nusu awe ametoa majibu kwa wananchi kama atasaini au hatasaini Mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo wataitisha maandamano nchi nzima ikiwa ni pamoja na kususia kuingia kwenye Bunge la Katiba
   Msimamo huo ulitolewa Dar es Salaam jana kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Jangwani na kuudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini.

Akihutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema Rais Kikwete, anatakiwa awe amejibu madai yao ndani ya muda huo vinginevyo yatafanyika maandamano hayo.

Mbowe alisema wataitisha maandamano hayo Oktoba 10, mwaka huu na hawataenda Polisi kuomba kibali isipokuwa watatoa taarifa kwani IGP Said Mwema ameelezwa jambo hilo.

Alisema safari hii hawatakuwa tayari kuitwa kwenda Ikulu kuzungumzia suala hilo kwa sababu hata madai yao ya awali waliyokubaliana na Rais Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam hakuna kilichofanyiwa kazi.

“Hatutakuwa tayari kwenda Ikulu kunywa chai wala juisi kwani hata makubaliano ya awali kuhusu mswada huo hakuna kilichofanyika,” alisema Mbowe. Alisema madai yao yote Rais Kikwete anayafahamu hivyo hawarudi kujadili suala hilo badala yake wanataka majibu ya madai yao.

Alisema kwa sasa hatua ambazo tayari wamechukua ni kwenda kuona makundi mbalimbali ya kijamii nje ya wanasiasa ili kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kwa kuamini kuwa wananchi ndiyo msingi wa katiba.

Mbowe alisema migogoro ya ardhi inayoendelea nchini inachangiwa na Katiba, hivyo lazima ipatikane katiba ambayo itakuwa suluhisho la matatizo hayo. “Kosa kubwa kati ya makosa yote ni woga wa kudai haki, kinachotakiwa kwa sasa ni ujasiri,” alisema na kuongeza kwamba, kuwa na watu wenye woga ndiyo chanzo cha kuwa na katiba mbovu.

Mbatia

Kwa upande wake Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia, alisema katiba ni kitendo cha maridhiano na wala si cha kibabe kama CCM inavyotaka kufanya, hivyo watahakikisha inapatikana kwa gharama yoyote.

Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zinakinzana kwenye suala la madaraka ya rais. Alitoa mfano kuwa Katiba ya Zanzibar inamnyang’anya Rais wa Jamhuri ya Muungano madaraka katika suala la kuigawa nchi na hiyo inaonesha wazi kuwa kuna mgogoro wa kikatiba.

“Inabidi ieleweke kuwa, Tanzania kwanza vyama baadaye...ieleweke kuwa CCM itayeyuka lakini Tanzania itabaki,” alisema na kuongeza kwamba ieleweke wazi kwamba, nchi sasa tayari ipo kwenye mgogoro wa kikatiba.

Alisema katiba inatakiwa itokane na wananchi wenyewe na si kuhodhiwa na chama kimoja cha CCM na wananchi kupoteza haki ili kupata katiba bora kwa ajili ya miaka 100 ijayo.

Prof. Lipumba

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema CCM inatumia ubabe hadi ndani ya Bunge kiasi cha kufikia hatua ya wabunge wanapigwa. “Hiki ni kielelezo kuwa umefika wakati wa kuanza kufanya mazoezi ya viungo,” alisema na kuongeza kuwa tunahitaji kupata katiba inayohakikisha rasilimali za Tanzania zinatumika kwa manufaa ya wananchi wote.

Aliongeza kuwa mswada uliopelekwa bungeni hauna ridhaa ya wananchi na umepitishwa kwa kuvunja katiba ya sasa ambayo inaeleza kuwa unatakiwa upitishwe na wabunge zaidi ya theluthi mbili, lakini idadi hiyo haikufika mswada ukapitishwa.

Prof. Lipumba alisisitiza kuwa wananchi wa Zanzibar hawakushirikishwa kutoa maoni yao.

“Makamu wa pili wa Rais Zanzibar alidhalilishwa kwani alipigiwa simu na waziri Mkuu Mizengo Pinda, ili aende Dodoma na baada ya kufika mswada wenye vipengele 11 vimepitishwa na vitano vimeongezwa ambavyo hajawahi kuviona,” alisema Prof. Lipumba na kusisitiza kuwa; “CCM wabaya! Wanamdhalilisha hata mwana-CCM mwenzao?”

Askofu Kakobe

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe, alimtaka Rais Kikwete asisaini mswada huo; na akifanya hivyo atakuwa ameshindwa mtihani mkubwa wa kitaifa kwani suala hilo lipo mikononi mwake.

Alisema mwanzo alionesha njia nzuri kwa kukubali mchakato wa Katiba mpya na iwapo atasaini wataona ilikuwa danganya toto. Alisisitiza kuwa makundi ya jamii hayajashirikishwa.
“Katiba ya kweli inaanza na sisi wananchi ambao ndio chimbuko la viongozi wote na 
 

Shekhe Kitimba
Naye msemaji wa Shiah ya Maimamu Shekhe Rajabu Kitimba ; “Hili la katiba ni letu, haki haiombwi na sisi tunaunga mkono viongozi wote kwa asilimia 100.”
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa pamoja na wale wa dini ambapo walitoa matamko ya kumtaka Rais Kikwete asisaini mswada huo.

2 comments:

  1. Heee mpaka Kakobe yumo! Vipi alivyojitajirisha kwa kufisadi watu kwa njia ya kiroho? Leo yuko jukwaani bila haya akimshurutisha rais alyechaguliwa kihalali na watu kufanya jambo asilolitaka!

    ReplyDelete
  2. Heee mpaka Kakobe yumo! Vipi alivyojitajirisha kwa kufisadi watu kwa njia ya kiroho? Leo yuko jukwaani bila haya akimshurutisha rais alyechaguliwa kihalali na watu kufanya jambo asilolitaka!

    ReplyDelete