25 September 2013

CAG KUKAGUA OFISI YA MEYA BUKOBA



 Mariam Mziwanda na Stella Aron
   Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Ludovick Utouh, amesema ofisi yake ipo mbioni kwenda mjini Bukoba, mkoani Kagera, ili kufanya ukaguzi wa mahesabu katika Ofisi ya Meya na kutoa ripoti yenye uhakika.
  Bw. Utouh aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mafunzo yaliyoshirikisha Wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari ili kuwajengea uwezo wa kuripoti taarifa za ofisi hiyo.
  Alisema ukaguzi wanaokwenda kuufanya mjini Bukoba, hautokani na matakwa ya Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Nape Nnauye; bali ni ombi maalumu lililotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
  Aliongeza kuwa, kumekuwa na taarifa za upotoshaji ambazo zimekuwa zikifanywa na baadhi ya makundi ambayo hayana nia njema na ofisi hiyo, hivyo ni vyema ikaeleweka kuwa, ukaguzi huo umezingatia agizo la Waziri Mkuu.
 "Ofisi yangu inafanya kazi kikatiba si kwa matakwa ya chama chochote cha siasa, ukaguzi maalumu ambao utafanyika mjini Bukoba, utaanza wiki ijayo...ni jukumu la vyombo vya habari kuwa waangalifu wanaporipoti taarifa hizi.
 "Wananchi wa Bukoba wasiwe na wasiwasi, tunakwenda huko lakini hatutaki chai ya mtu labda usafiri ambao upo kisheria kwa ajili ya ukaguzi wa miradi yenye utata iweze kufikiwa na kupatikana taarifa sahihi," alisema.
  Bw. Utouh alisema uwajibikaji na uwazi ni mambo yasiyoweza kupatikana katika mfumo wa kuficha taarifa za utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali.
  Alisema mahali ambapo habari inafichwa, lazima patatokea mvutano, kutoaminiana na hatimaye wananchi kuona Serikali yao ndiyo chanzo cha matatizo hivyo ni muhimu haki ya kikatiba kwa wananchi kupashwa habari ikazingatiwa.
  Alitumia fursa hiyo kuvitaka vyombo vya habari nchini k u p u n g u z a u p o t o s h a j i n a kuelimisha jamii ipasavyo ili kusaidia makundi mbalimbali kuzielewa vizuri ripoti za CAG ili kuzuia machafuko yasiyo na lazima nchini.
 "Madhara ya kuripoti taarifa za upotoshaji na mipaka ambayo inahitajika ni makubwa kwa jamii ...tunahitaji kufikiria masuala mazito yanayokwamisha kufikia malengo yetu, hivyo ni muhimu kuacha kutoa taarifa zisizo sahihi," alisema

No comments:

Post a Comment