29 August 2013

YANGA YAKWAA KISIKI SIMBA SC YATAKATA



 Na Elizabeth Mayemba
MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana wamekwaa kisiki baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Katika mechi ya ufunguzi wa ligi hiyo, Yanga iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu Ashanti United.

Mchezo ulianza kwa timu hizo kusomana taratibu lakini, Coastal Union ilianza kufika lango la Yanga ambapo dakika ya 17, Jerry Santo aliachia shuti kali akiwa nje ya 18 lakini mpira ukapaa juu ya lango.Dakika ya 23 lango la Yanga lilikuwa katika hekaheka tena baada ya Coastal Union kuliandama lango la mabingwa hao ambapo, Yayo Litumba aliwatoka mabeki wa mabingwa hao na kuachia shuti kali ambalo lilipanguliwa na Ally Mustafa 'Bathez' na kuwa kona tasa.
Baada ya mashambulizi hayo, Yanga iliamka na kuliandama lango ya Coastal Union ambapo dakika ya 35 Nadir Haroub 'Canavaro' alikosa bao la wazi baada ya kuachia shuti kali lililopaa juu ya lango.Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana, huku Coastal Union ikikosa nafasi nyingi za kufunga.
Baada ya timu kurudi uwanjani kipindi cha pili, Yanga ilicharuka na kufanikiwa kupata bao dakika ya 65 kupitia kwa Didier Kavumbagu, baada ya kuunganisha krosi ya David Luhende.Dakika ya 75 mwamuzi wa mchezo huo, Martin Saanya aliwatoa nje kwa kadi nyekundu wachezaji, Christine Odula na Simon Msuva kwa kuchezeana rafu.
Wakati mashabiki waliohudhuria mechi hiyo wakidhani mchezo huo ungemalizika kwa Yanga kutoka na ushindi, Coastal ilipata bao la kusawazisha kupitia kwa Santo kwa mkwaju wa penalti baada ya beki mmoja wa Yanga kuunawa mpira katika eneo la hatari.Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, iliyopigwa jana jijini Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji JKT Oljoro.
Simba katika mechi ya ufunguzi ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Rhino Rangers ya Tabora ambayo imepanda daraja msimu huu.Bao la Simba lilipatikana dakika ya 34 lililowekwa kimiani na Haroun Chanongo kwa shuti lililomshinda kipa wa JKT Oljoro.
Hata hivyo dakika ya 50, Issa Kanduru wa JKT Oljoro alikosa penalti baada ya beki wa Simba, George Owino kuunawa mpira katika eneo la hatari akiwa katika harakati za kuokoa.Kutoka Mbeya, Charles Mwakipesile anaripoti kuwa timu ya Mbeya City ilipata ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya JKT Ruvu katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Sokoine.


No comments:

Post a Comment