- YAIFYATUA MABAO 4-1 TAIFA
Na Elizabeth Mayemba
MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga jana walidhihirisha kwamba ni
mabingwa wa kweli, baada ya kuinyuka SC Villa ya Uganda mabao 4-1, katika mechi
ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Waganda hao juzi
pia walipokea kichapo cha mabao kama hayo kutoka kwa Simba katika mechi ya
kirafiki ya kimataifa iliyochezwa katika uwanja huo huku 'Wekundu'
wakiadhimisha siku yao ya 'Simba Day' inayofanyika kila mwaka.
Mpira ulianza
kwa kasi kwa timu zote kushambuliana lakini, Yanga ndiyo ilianza kupata bao la
kwanza dakika ya saba lililokwamishwa kimiani na Mrisho Ngassa, kwa shuti la
mbali lililomshinda kipa wa SC Villa, Elungat Martin.
Villa ilisawazisha
bao hilo dakika ya 18 kupitia kwa Siraj Jamal, baada ya kutokea piga nikupige
langoni mwa Yanga huku mabeki wake wakishindwa kuokoa hatari hiyo.
Nadir Haroub 'Canavaro' aliipatia Yanga
bao la pili dakika ya 27, baada ya kuachia shuti la mbali baada ya kupokea pasi
fupi ya Haruna Niyonzima aliyepiga mpira wa faulo langoni mwa Villa.
Yanga iliendelea kuliandama lango la
wapinzani wao ambapo mshambuliaji, Didier Kavumbagu aliwapatia mabingwa hao wa
Tanzania Bara bao la tatu dakika ya 30 akimalizia shuti lililopigwa na Jerry
Tegete, lililogonga mwamba wa lango la Villa na kumkuta mfungaji.
Katika kipindi hicho Villa ambayo juzi
ilinyukwa mabao 4-1 na Simba, walizidiwa kila idara na kuruhusu washambuliaji
wa Yanga, kulitia misukosuko lango lao mara kwa mara.
Kipindi cha pili Yanga, waliingia kwa
kasi huku Kavumbagu akikosa bao dakika ya 50, baada ya kuachia shuti kali
lililotoka nje kidogo ya lango la Villa.
Yanga iliongeza bao la nne dakika ya 61
lililopachikwa na Niyonzima, aliyetoka na mpira katikati ya uwanja na kuachia
shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.
No comments:
Post a Comment