15 August 2013

YANGA, AZAM FC ZAINGIA MSITUNI



 Na Elizabeth Mayemba
HOMA ya pambano la Ngao ya Jamii imezidi kupamba moto, baada ya Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga jana kuingia kambini Makao Makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Kila mwaka bingwa wa ligi kuu ambapo safari hii ni Yanga na mshindi wa pili Azam FC huwa wanacheza mechi hiyo maalum ya kufungua msimu mpya wa ligi kuu.

Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini inatarajiwa kufanyika Agosti 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana Msemaji wa klabu ya Yanga Baraka Kizuguto, alisema timu yao tayari imeshaingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo huku wachezaji wakiendelea kufanya mazoezi.
"Timu yetu imeshaingia kambini hapa Makao Makuu ya klabu yetu na wachezaji wanaendelea na mazoezi kama kawaida kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo ambalo linatarajiwa kuwa na upinzani mkali," alisema Kizuguto.
Alisema kwa upande wao wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mpambano huo na lengo lao ni kuifunga Azam FC na kutwaa taji hilo.
Kwa upande wa wapinzani wao Azam FC waliorejea juzi kutoka Afrika Kusini walipoweka kambi ya wiki mbili, wao wapo kwenye klabu yao , Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mchezo huo wa kuashiria kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara umeteka hisia za wengi na kila timu inaonekana kupania kushinda ili kuwasha taa za kijani kuelekea mbio za ubingwa.
Yanga iliifunga Azam FC katika mechi zote tatu za msimu uliopita.
Yanga watakuwa na hasira za kutaka kulipa kisasi kwa timu hiyo ambayo imekuwa ikiwasumbua, lakini safari hii wamepania kuanza kuifunga kuanzia Ngao ya Jamii hadi kwenye ligi kuu.
Katika kujiandaa na msimu, Yanga walicheza mechi saba za kirafiki na kushinda tatu, kufungwa moja na sare tatu.Walizifunga Mtibwa Sugar 3-1, SC Villa ya Uganda 4-1 na 3Pillars ya Nigeria 1-0, na kutoa sare ya 1-1 na Express, 2-2 na URA zote za Uganda na 0-0 na Rhino FC mjini Tabora, wakati walifungwa 2-1 na Express ya mjini Shinyanga.
Kwa Azam kabla ya kwenda Afrika Kusini walicheza mechi nne na kushinda tatu, 1-0 na kombaini ya JKT, 4-0 na African Lyon na 5-1 Ashanti United.
Na ikiwa Afrika Kusini, ilicheza mechi nne na kufungwa tatu na kushinda moja, ilifungwa 3-0 na Kaizer Chiefs, 2-1 na Orlando Pirates na 1-0 na Moroka Swallows, wakati yenyewe ilishinda 1-0 dhidi ya Mamelodi Sundown

No comments:

Post a Comment