20 August 2013

WIZARA YAANZA KUTOA ELIMU YA WANYAMAPORINa Daud Magesa, Mwanza
WIZARA ya Maliasili na Utalii, Idara ya Wanyamapori kwa kutumia wataalamu wake, inafanya ziara ya kutembelea na kutoa elimu kwenye maeneo yenye matatizo ya fisi wanaoua watu hasa watoto wadogo katika vijiji vya Masemele na Chabakima katika mikoa ya Mwanza na Geita.

Akizungumza na gazeti hili jana mwakilishi wa wizara hiyo,Twaha Twaibu alisema ziara hiyo imelenga kubaini chanzo cha tatizo na kutoa elimu kwa wananchi kwa njia ya mikutano pamoja na kuwaonesha sinema za wanyamapori kuhusu tabia za wanyama hao ambayo itahitimishwa Agosti 25, mwaka huu .
Alisema kutokana na kuongezeka kwa matukio ya wanyamapori kushambulia na kuua binadamu hasa watoto wadogo kwenye maeneo mengi ya Mkoa wa Mwanza, Geita na Simiyu,Wizara imewatuma wataalamu hao kuelimisha wananchi kuhusiana na kadhia hiyo
Bw.Twaha Twaibu ambaye ni Mkuu wa Uenezi wa Idara ya Wanyamapori Dar es Salaam pamoja na Benjamini Kijika ambaye ni mkuu wa kikosi dhidi ya ujangili Kanda ya Ziwa wamesema kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali, ambapo kwa kipindi cha mwaka jana na hadi sasa jumla ya fisi 11 wameuawa na kikosi hicho.
Bw.Twaibu alisema kwa baadhi ya wananchi waliopata matatizo wizara iliweza kuwalipa na inaendelea na mchakato wa kuwalipa wananchi wengine waliopatiwa na matatizo.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2012/13 pekee kufikia Juni,2013, familia 93 zililipwa kifuta machozi cha sh. 49,200,000 kwa wananchi waliojeruhiwa na wanyama wakali wakiwemo fisi kwa nchi nzima.
Akiwa katika vijiji vya Masemele na Chabakima, Twaibu alitoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu katika ziara hiyo iliyoanza jana, kwenye vijiji vya Masemele na Chabakima, katika kata ya Bugogwa katika Wilaya ya Ilemela, Mkoa wa Mwanza na itaendelea katika maeneo mengine kama Wilaya za Magu na Geita.
"Kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Serikali ,ninawapa pole familia za wananchi wote wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa matatizo yaliyowapata ya kujeruhiwa au kupoteza ndugu zao wapendwa.Wizara imekuwa ikitoa kifuta machozi kwa kuwalipa wananchi waliojeruhiwa na kuuawa na wanyamapori wakali wakiwepo fisi na itaendelea kufanya hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 71 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009," alisema Twaibu.
Bw.Benjamini Kijika aliwaeleza wananchi hao kuwa suala la kusaka fisi limekuwa na vikwazo ambavyo yeye kama mtaalamu wameshindwa kuelewa na kuhisi kuna masuala ya ushirikina kuhusu fisi hao.
Alisema alipoitwa na kuelezwa kuwa fisi wameonekana kijijini na kufanya msako, wanyama hao hawakuonekana wala kusikia sauti ya wanyama hao hata walipofuatilia zaidi hawakufanikiwa kuwaona na wakati mwingine waliwahi kuelezwa na wananchi Wilaya ya Ilemela kijiji cha Muhonzi kuwa fisi ameua mtoto wa shule na wananchi walimsaka na kumuua fisi huyo.
Hata hivyo alidai kushangazwa mara baada ya askari wanyamapori kufika eneo la tukio hawakuona dalili zozote za damu wala mikwaruzo ya alama ya mtoto na nyayo za fisi, isipokuwa waliona nguo za mtoto huyo aliyekamatwa na fisi zikiwa zimetundikwa juu ya mti zikiwa hazina hata damu wala kuchanwa, kitu ambacho ni tofauti na tabia za mnyama huyo anaposhambulia binadamu.
Kijika aliwaomba wananchi kusaidia kukabiliana na tatizo hilo na inawezekana vipo vitendo vya ushirikina vinafanyika, na kama vipo waviache.
Hivi karibuni gazeti la Mzawa toleo la Agosti 17 mwaka huu,lilikuwa na kichwa cha habari 'Fisi wahusishwa na Ushirikina Bariadi', likieleza jinsi jeshi la Sungusungu la kijiji cha Ng'hesha walivyolazimika kuwacharaza viboko akinamama vikongwe, wakitaka kubaini chanzo cha matukio hayo.

No comments:

Post a Comment